Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma Adv.Marry Makondo Akizungumza katika uzinduzi wa MsingiTek uliofanyika Mkoani Ruvuma kwa lengo la kuboresha ujifunzaji wa wanafunzi wa shule za msingi 
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Mkoa wa Ruvuma umezindua rasmi mradi wa MsingiTek unaotumia teknolojia ya kidijitali kuboresha ujifunzaji wa wanafunzi wa shule za msingi, hususani katika stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), huku mpango huo ukilenga kufikisha huduma hiyo katika shule 100 za mkoa huo ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026.
Uzinduzi wa mradi huo umefanyika katika shule ya msingi Humbaro na kufanywa na katibu tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Adv. Mary Makondo, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, Brigedia Jenerali Ahmed Abasi Ahmed.
Akizungumza katika hafla hiyo, Makondo amesema MsingiTek ni miongoni mwa afua zinazolenga kuboresha mazingira na mbinu za ujifunzaji kwa kutumia teknolojia, hatua inayokwenda sambamba na juhudi za Serikali katika kuimarisha ubora wa elimu nchini.
Makondo pia amelipongeza Shirika la Imagine Worldwide pamoja na wadau wake, akiwemo TanzaEducation, kwa kuwezesha teknolojia hiyo kuwafikia wanafunzi katika shule mbalimbali za Ruvuma, ikiwemo zile zilizopo maeneo ya pembezoni.
Amesema Serikali inatambua mchango wa sekta binafsi katika kuunga mkono jitihada za kuboresha huduma za elimu, huku akiwashukuru Imagine Worldwide na Onebillion kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa programu hiyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Imagine Worldwide, Deo Chuwa, amesema MsingiTek ilizinduliwa nchini Tanzania Mei 2025 kwa lengo la kuimarisha ujifunzaji wa msingi kwa watoto kupitia teknolojia inayoweza kutumika bila kuhitaji mtandao.
Amesema kwa sasa programu hiyo inatekelezwa katika shule za msingi za Serikali 250 zilizopo katika mikoa mitano na wilaya 11, ikiwafikia zaidi ya wanafunzi 57,000.
Chuwa amesema programu hiyo inalenga kupanuka na kufikia shule 500 zitakazohudumia zaidi ya wanafunzi 120,000 nchini, huku Ruvuma ikilenga kufikisha MsingiTek katika shule 100 ifikapo mwishoni mwa mwaka 2026.
Ameeleza kuwa hatua hiyo itaongeza fursa kwa wanafunzi wengi zaidi kutumia teknolojia katika kuimarisha stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.




Social Plugin