Na Dotto Kwilasa, Dodoma
Jeshi la Polisi nchini limetumia Maonesho ya Biashara na Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya Dk. John Samuel Malecela mkoani Dodoma kuimarisha ulinzi na usalama, huku likitoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na jeshi hilo kwa lengo la kuongeza uelewa na kuimarisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya uhalifu.
Akizungumza katika maonesho hayo Leo Agosti 6,2026 Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma Kamishina msaidizi (ACP) wa polisi Gallus Hyera amesema ushiriki wa jeshi hilo unatokana na wajibu wake wa kikatiba na kisheria wa kulinda amani, usalama wa raia na mali zao, kusimamia utekelezaji wa sheria, kupeleleza makosa ya jinai pamoja na kuwakamata wahalifu.
Amefafanua kuwa mkoa wa Dodoma unaendelea kuwa salama kutokana na mikakati mbalimbali inayotekelezwa na Jeshi la Polisi ikiwemo doria, misako na operesheni maalum, sambamba na kuimarisha ulinzi ndani na nje ya viwanja vya maonesho ili kuhakikisha wananchi na wageni wanashiriki Nanenane kwa utulivu na usalama.
Aidha, amesema Jeshi la Polisi limetenga mabanda maalumu yanayotoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma mbalimbali zinazopatikana katika vituo vya polisi, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa huduma hizo na kujenga uelewa wa sheria na taratibu za usalama.
Ametaja baadhi ya maeneo yanayotolewa elimu kuwa ni Chumba cha Mashtaka, Polisi Jamii, Polisi Mtandao, Kitengo cha Alama za Vidole, usalama barabarani, udhibiti wa madawa ya kulevya, makosa ya mtandao, haki za binadamu, Polisi Mazingira, Madini na Maliasili, pamoja na Dawati la Jinsia na Ulinzi wa Mtoto.
Pia wananchi wanapatiwa elimu kuhusu madhara ya umiliki haramu wa silaha, kuzuia wizi wa mifugo kupitia Kitengo cha STU, matumizi ya mbwa na farasi wa polisi katika utekelezaji wa majukumu ya kiusalama, pamoja na nafasi ya ushirikishwaji wa jamii katika kuzuia uhalifu.
Katika hatua nyingine, Jeshi la Polisi limeeleza kuwa linaendelea kushirikiana na waganga wa tiba asili wanaoshiriki maonesho hayo kwa kuwataka kuzingatia sheria za nchi wakati wa kutoa huduma zao na kuepuka vitendo vya ramli chonganishi vinavyoweza kuchochea uhalifu au migogoro.
Vilevile, waganga hao wamehimizwa kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi endapo watabaini watu wanaotuhumiwa kutenda makosa ya jinai wakifika kwao wakitafuta huduma za kujikinga dhidi ya hatua za kisheria.
Jeshi la Polisi limetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana nalo kwa kutoa taarifa za uhalifu, huku likiwashukuru wote waliotembelea banda lake katika Maonesho ya Nanenane na kuahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa lengo la kuimarisha usalama na amani nchini.



Social Plugin