Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

PBZ NA TADB WAWAWEZESHA WAKULIMA KUPATA MITAJI YA PEMBEJEO

Jengo la ofisi ya watu wa Zanzibar tawi la Mbeya (PBZ)linaloshirikiana na benki ya maendeleo ya kilimo Tanzania (TADB)lenye lengo la kuwawezesha wakulima kupata mikopo ya pembejeo Nyanda za juu kusini na mikoa ya kusini mwa Tanzania 
Wafanyakazi wa benki ya watu wa Zanzibar( PBZ)katika majukumu yao ya kila siku 

Na Regina Ndumbaro-Mbeya

Ushirikiano kati ya Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) na Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) umeendelea kuwawezesha wakulima kupata mikopo ya kugharamia mahitaji muhimu ya kilimo, ikiwemo pembejeo, katika Nyanda za Juu Kusini na mikoa ya kusini mwa Tanzania.

Kaimu Meneja wa Tawi la PBZ jijini Mbeya, Abdul Haruni, amesema mfumo huo umewapa wakulima fursa ya kupata mitaji kupitia mgawanyo wa fedha ambapo PBZ huchangia asilimia 40 ya mkopo na TADB asilimia 60.

Akizungumza na  Malunde 1-Blog ofisini kwake, Haruni amesema miongoni mwa walionufaika na mfumo huo ni wakulima wa zao la korosho, ambapo wakulima wapatao 20 wamepata mikopo kwa ajili ya kuimarisha shughuli zao za kilimo.

Amesema mpango huo ni sehemu ya juhudi za kuongeza upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wakulima ambao mara nyingi huhitaji mitaji mikubwa kwa ajili ya pembejeo na mahitaji mengine ya uzalishaji.

“Lengo ni kuhakikisha kwamba mkulima anapata mahitaji yake muhimu ya pembejeo za kilimo,” amesema Haruni.

Amesema uwepo wa PBZ katika Mkoa wa  Mtwara, na Nyanda za Juu Kusini umeongeza wigo wa huduma za kifedha kwa wakulima na wafanyabiashara katika maeneo hayo.

Kwa mujibu wa Haruni, PBZ ilianzishwa Juni 30, 1966 chini ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na imekuwa ikifanya kazi Zanzibar na Tanzania Bara.

Amesema kwa upande wa Zanzibar benki hiyo inafanya kazi kwa asilimia 99 na Bara kwa asilimia 12, huku ikitoa huduma kwa misingi ya sheria za Kiislamu na sheria za kimataifa.

Haruni amesema PBZ ilianza kufanya kazi Mtwara mwaka 2011, huku tawi la Mbeya likianzishwa Juni 2024 kwa lengo la kuwafikia zaidi wananchi, wakiwemo wakulima.

Amesema mbali na mikopo ya kilimo, benki hiyo pia hutoa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo, ikiwa ni sehemu ya kuwawezesha wananchi kupata mitaji na kuendeleza shughuli zao za kiuchumi.

Amesema viwango vya riba kwa mikopo hiyo vinatajwa kuwa kati ya asilimia 14 hadi 16, huku benki ikiendelea kutoa huduma za kifedha kupitia matawi na mawakala.

Haruni amesema benki hiyo pia imekuwa ikitoa elimu kwa wafanyabiashara wa madini katika maeneo ya machimbo ya Chunya kuhusu umuhimu wa kuhifadhi fedha katika taasisi za fedha badala ya kuzitunza majumbani au kwenye vibubu.

Amesema hatua hiyo inalenga kupunguza hatari zinazoweza kusababisha hasara, ikiwemo wizi, moto wa nyumba na majanga mengine.

Ameeleza kuwa wakati wafanyabiashara wanapokabiliwa na changamoto za mitaji, benki imekuwa ikiwapa fursa ya kukopa, akitolea mfano kipindi cha janga la Corona ambapo baadhi ya wafanyabiashara waliokuwa wameishiwa mitaji walipatiwa mikopo ya kuendeleza biashara zao.

Aidha, Haruni amesema PBZ imeendelea kutoa akaunti kwa makundi mbalimbali, ikiwemo STARA kwa wastaafu, MREMBO kwa akina mama, pamoja na akaunti za watoto na wanafunzi.

Amesema huduma hizo zimekuwa zikitumiwa pia na watumishi wa umma, ambao baadhi yao wamekuwa wakitumia benki hiyo kupata mikopo na huduma nyingine za kifedha, huku baadhi wakiendelea kunufaika baada ya kustaafu kupitia akaunti ya STARA.

Kwa upande wa vijana wanaojiandaa kuingia katika sekta ya fedha, Haruni amesema tawi la PBZ Mbeya limepokea zaidi ya wanafunzi 16 wanaofanya mafunzo kwa njia ya vitendo (Field), wakijifunza shughuli mbalimbali za benki.

Haruni ameishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ushirikiano wanaoutoa, akisema dira ya PBZ ni kuendelea kuenea katika maeneo mengi ndani na nje ya nchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com