Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

MIRADI YA ZAIDI YA MILIONI 644 YATEKELEZWA NAMTUMBO HOMERA AMSHUKURU RAIS SAMIA

Mbunge wa Jimbo la Namtumbo na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera akizungumza na wananchi wa Namtumbo wakati wa ziara yake ambayo imeanza jana katika kata za Hanga na Mputa Namtumbo ikilenga kukagua miradi yenye thamani ya shilingi milioni 644 na kusikiliza kero za wananchi 
Moja ya mawe yaliyowekwa  na Mbunge wa Jimbo la Namtumbo na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Juma Zuberi Homera 

Na Regina Ndumbaro Namtumbo 

Mbunge wa Jimbo la Namtumbo na Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Zuberi Homera, amesema wananchi wa Namtumbo wanaendelea kushuhudia maendeleo makubwa kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, huku akimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuwezesha upatikanaji wa fedha za miradi hiyo.

Dkt. Homera ameyasema hayo Agosti 12, 2026, wakati wa ziara yake ya kikazi katika kata za Hanga na Mputa, ambapo alikagua na kuweka mawe ya msingi katika miradi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 644, huku akisikiliza kero na changamoto za wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

 Katika kata ya Hanga, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa madarasa sita katika shule ya msingi Dkt. Homera, eneo la Mageuzi, mradi wenye thamani ya shilingi milioni 144 unaotarajiwa kukamilika septemba 11, 2026.

 Baada ya hafla hiyo, amefanya mkutano na wananchi, amesikiliza kero zao na pia kuwasalimia wananchi waliojitokeza barabarani katika maeneo ya Mawa na Hanga kati.

Katika kata ya Mputa, Dkt. Homera ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa Kituo cha Afya Mputa kinachogharimu shilingi milioni 500. 

Kituo hicho kitakapokamilika kitakuwa na jengo la wagonjwa wa nje (OPD), jengo la huduma za mama na mtoto pamoja na jengo la upasuaji, huku ujenzi wake ukitarajiwa kukamilika Oktoba 24, 2026. 

Aidha, katika ziara hiyo amekabidhi gari la wagonjwa (ambulance) kwa ajili ya kuimarisha huduma za afya na kuwezesha wananchi kupata huduma za dharura kwa wakati.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Dkt. Homera amewashukuru wananchi wa Namtumbo kwa ushirikiano wao na kumpongeza kwa dhati Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa fedha zinazotumika kutekeleza miradi ya maendeleo katika jimbo hilo. 

Amesema ziara hiyo itaendelea Agosti 13, 2026, katika Kata za Mputa na Kitanda, ambapo ataendelea kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com