Na Marco Maduhu, SHINYANGA
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad, ameendelea na ziara yake ya kusikiliza kero za wananchi na kuzitolea majibu, akiwa ameambatana na wataalamu mbalimbali wa Serikali.
TAZAMA VIDEO👇👇
Leo Agosti 5, 2026, Mbunge Azza amefanya ziara katika Kijiji cha Ilobashi, Kata ya Masengwa na Ng'wanhalanga, wilayani Shinyanga.
Akizungumza wakati wa kujibu kero mbalimbali za wananchi, likiwamo ombi la kusaidia ujenzi wa nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Ilobashi kwa kutoa mifuko ya saruji, Mbunge Azza ameahidi kutoa mifuko 150 ya saruji.
"Mimi kama Mbunge ninaahidi kutoa mifuko 150 ya saruji ili kuunga mkono ujenzi wa nyumba hiyo ya walimu katika Shule ya Msingi Ilobashi. Afisa Elimu, nitakapoleta mifuko hiyo ya saruji kwa ajili ya kumalizia sehemu ya juu ya jengo, na halmashauri nayo iangalie namna ya kukamilisha ujenzi wa nyumba hiyo," amesema Azza.
Aidha, akijibu kero ya ukosefu wa maji, ameiomba Wakala wa Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) kutatua tatizo la maji katika Kijiji cha Ilobashi na kuhakikisha huduma hiyo inafika pia katika vitongoji ambavyo bado havina maji.
"Jimbo la Itwangi lina vijiji 58, ambapo vijiji 34 havina hata maji ya kisima. Kwa nini Ilobashi kuna tanki la maji lakini wananchi hawapati huduma hiyo? Mimi kama Mbunge sitakubaliana na hali hiyo. naomba RUWASA mhakikishe Ilobashi yote inapata maji," amesema Azza.
Aidha, amesema katika suala la umeme Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) inasema kuanzia 2025 hadi 2030 vitongoji vyote vitakuwa na umeme, na kwamba ndani ya miezi sita ya utendaji kazi ya serikali ya awamu ya sita chini Mheshimiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwamba katika Kijiji cha Ilobashi watawekewa umeme kwenye vitongoji viwili cha Mwajilenge na Ilebelo.
“Wataalamu wa REA wameshafika na kufanya tathimini na muda wowote mtaona nguzo zinashuka kwenye maeneo yenu,” amesema Azza.
Awali Mwenyekiti wa Kamati ya shule ya Msingi Ilobashi Hamis Nyelesa, amemuomba Mbunge Azza, kusaidia ujenzi wa Jengo la nyumba ya walimu katika shule hiyo ambalo lipo usawa wa dirisha, kwamba awasaidie mifuko ya saruji ili kumalizia jingo hilo.
Mwananchi Mwingine Elias Charles, anasema kwenye Kijiji hicho kuna kero kubwa ya maji, ambapo yamekuwa yakikatwa ndani ya wiki moja hadi mbili na yakirudi usiku wasaa 8 na saa 12 Alfajiri yanakata.
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad yupo katika ziara ya kushukuru wananchi pamoja na kusikiliza kero mbalimbali za wananchi wa jimbo hilo.
TAZAMA PICHA👇👇
Mbunge wa Jimbo la Itwangi Azza Hillal Hamad akizungumza.
Diwani wa Masengwa Nicodemas Simon akizungumza.
Social Plugin