Meneja wa mfuko wa bima ya afya Mkoa wa Ruvuma Hansi John wa kwanza kutoka kushoto akiwa katika picha ya pamoja na MANTRA Tanzania Ltd baada ya kampuni ya MANTRA Tanzania Ltd inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya urani wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma kutoa kadi za bima ya Afya kwa wanafunzi 1,000
Meneja wa mfuko wa bima ya afya Mkoa wa Ruvuma Hansi John Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake baada ya kutembelewa na kampuni ya MANTRA Tanzania Ltd katika kushirikiana na MANTRA Tanzania Ltd kuwawezesha wanafunzi 1,000 kuhakikisha wanapata huduma za uhakika ili kuweza kushiriki katika masomo yao Na Regina Ndumbaro, Songea-Ruvuma
Kampuni ya MANTRA Tanzania Ltd inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya urani wilayani Namtumbo mkoani Ruvuma, imetoa zaidi ya shilingi milioni 50 kugharimia Bima ya Afya kwa Wote kwa wanafunzi 1,000 wa Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wake wa uwajibikaji kwa jamii.
Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 21, 2026 katika Ofisi za Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Mkoa wa Ruvuma, Afisa Mahusiano wa MANTRA Tanzania Ltd, Yahanis Kilave, amesema kampuni hiyo ina vipaumbele mbalimbali katika kusaidia jamii, ambavyo ni afya, maji, elimu, michezo na vinginevyo.
Amesema wameona umuhimu wa kushirikiana na NHIF kuhakikisha wanafunzi hao wanapata uhakika wa huduma za afya ili waweze kushiriki katika masomo yao vizuri.
Kilave amesema MANTRA Tanzania Ltd inaamini kuwa baada ya wanafunzi hao kupata bima za afya wataweza kuzingatia masomo, kufanya vizuri na baadaye kuwa sehemu ya watu ambao kampuni itawahitaji.
“Tuna imani baada ya kutoa bima hizi watazingatia masomo yao watafanya vizuri ili tupate watu tutakaowahitaji baadaye,” amesema Kilave.
Aidha, amewashukuru watumishi wa NHIF kwa kazi kubwa waliyoifanya katika kufanikisha zoezi hilo, akisema licha ya kuwa lilikuwa zito, walijitahidi kulitekeleza kwa wakati na pale changamoto zilipojitokeza waliwasiliana kwa haraka.
Kwa niaba ya MANTRA Tanzania Ltd na Mkurugenzi wake Mkuu, Kilave ameushukuru uongozi wa NHIF, hasa Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Meneja wa Mkoa wa NHIF pamoja na wafanyakazi wake kwa kazi kubwa waliyoifanya, akisema wanaamini bima hizo zitawasaidia vijana kuzingatia elimu na kufanikiwa katika maisha yao.
Kwa upande wake, Meneja wa NHIF Mkoa wa Ruvuma, Hansi John, amesema mfuko huo una dhamana kwa wanaRuvuma na Watanzania kwa ujumla kuhakikisha wanakuwa na uhakika wa matibabu.
Amesema NHIF ina jukumu la kuwafikia watumishi wa umma, sekta binafsi pamoja na makundi makubwa ya wakulima kupitia AMCOS zao, wakiwemo wakulima wa kahawa, tumbaku na mahindi, huku watoto wakiwemo wanafunzi wakifikiwa kupitia Bima ya Toto ambayo gharama yake kwa mwaka ni shilingi 50,400.
Hansi amesema Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inalenga kuona kila Mtanzania anapata matibabu kwa kutumia bima ya afya na siyo fedha taslimu, kwa kuwa maradhi hutokea bila taarifa.
Ametumia nafasi hiyo kuishukuru MANTRA Tanzania Ltd kwa kufadhili bima hizo kwa wanafunzi 1,000 na kuzitaka kampuni nyingine kuiga mfano huo kwa kusaidia jamii na kurudisha kwa jamii kile wanachozalisha.
Hansi amesema kuwasaidia watoto kupata bima ya afya ni jambo muhimu kwa sababu mtoto anapokuwa na uhakika wa matibabu huondolewa hofu, hujawa na ujasiri na kujiamini, jambo linaloweza kumsaidia katika masomo na maisha yake kwa ujumla.
Katika tukio hilo, NHIF Mkoa wa Ruvuma imekabidhi cheti cha utambuzi kwa MANTRA Tanzania Ltd kwa kutambua mchango wa kampuni hiyo kwa jamii, ikiwemo uwezeshaji wa bima za afya kwa wanafunzi 1,000.
Aidha, Hansi John amemshukuru Mkurugenzi Mkuu wa NHIF Tanzania kwa kazi kubwa anayoifanya kuhakikisha Watanzania wanafikiwa na huduma za NHIF, hususan katika utekelezaji wa mpango wa Serikali wa Bima ya Afya kwa Wote


Social Plugin