Na Sheila Ahmadi, Dar es Salaam
Serikali imeeleza kuwa eneo la Kurasini Extension linatarajiwa kuanza kutumika kama sehemu ya Bandari ya Dar es Salaam ifikapo Novemba mwaka huu, hatua inayolenga kupunguza msongamano wa mizigo na malori katika Bandari ya Dar es Salaam.
Eneo hilo linatarajiwa kutumika kama Port Extension, ambapo mizigo itakayoshushwa katika Bandari ya Dar es Salaam itaelekezwa Kurasini Extension kwa ajili ya kuhifadhiwa, kukaguliwa na kusambazwa kwa maeneo mbalimbali.
Akizungumza Jijini Dar es salam Mara baada ya kutembelea bandari kavu iliyopo Kurasini Waziri wa Uchukuzi Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa Kurasini Extension linatarajiwa kuwa na uwezo wa kuhudumia hadi makasha 700,000 kwa mwaka, ikilinganishwa na uwezo wa sasa wa Bandari ya Dar es Salaam wa kuhudumia takribani makasha 344,000 kwa mwaka.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza uwezo wa bandari kuhudumia shehena kwa ufanisi, huku sehemu kubwa ya shughuli za mizigo ikihamishiwa katika eneo hilo na hivyo kupunguza presha katika eneo kuu la bandari.
"Mbali na kuhifadhi mizigo, Kurasini Extension litakuwa na eneo maalumu la maegesho ya malori, ambapo malori yatakayokuwa yakisubiri huduma yataingia ndani ya eneo hilo badala ya kusubiri kando ya barabara.Amesema Profesa Mbarawa".
Aidha Hatua hiyo inatarajiwa kupunguza msongamano wa malori katika barabara zinazozunguka Bandari ya Dar es Salaam na kuboresha mtiririko wa magari yanayohudumia shughuli za bandari.
Uhamishaji wa shughuli hizo kwenda Kurasini Extension unalenga kupunguza msongamano ndani ya bandari na kuwezesha mchakato wa ukaguzi wa mizigo kufanyika kwa ufanisi zaidi kabla ya mizigo kusafirishwa kwenda kwa wateja au kusafirishwa nje ya nchi.
Hata hivyo Barabara hiyo itaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kusimamia na kufuatilia usafirishaji wa mizigo kutoka bandarini kwenda Kurasini Extension, huku mifumo ya ulinzi na ufuatiliaji ikiwekwa kuhakikisha mizigo inafika salama na bila kukwepeshwa taratibu za forodha.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Wa Miundombinu,Mipango na uwekezaji Bandari ya Dar es Salaam Bw. Abed Gallus Abed amesema kuwa kukamilika kwa Kurasini Extension kutasaidia kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa mizigo na malori katika bandari hiyo.
Vilevile lengo ni kuhakikisha shughuli za ukaguzi, clearance na utoaji wa mizigo zinafanyika kwa ufanisi zaidi Kurasini Extension, jambo ambalo linatarajiwa kuongeza ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza muda wa kushughulikia mizigo.
Katika Hatua nyingine Kurasini Extension inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuongeza uwezo wa Bandari ya Dar es Salaam, kupunguza msongamano na kuboresha huduma kwa wafanyabiashara na watumiaji wa bandari.




Social Plugin