Na Sheila Ahmadi, Dar es Salaam
Kongamano la Tano la Uchumi wa Bluu linatarajiwa kuwakutanisha wadau kutoka ndani na nje ya Tanzania kujadili namna ya kutumia fursa za uchumi wa bluu kuongeza kipato cha wananchi na kuchochea ukuaji wa uchumi wa taifa.
Akizungumza Jijini Dar e s salaam na wanahabari kuhusu kongamano hilo, Mkuu wa Chuo cha Bahari Dar es Salaam (DMI) Profesa Tumaini Gurumo amesema kuwa uchumi wa bluu ni miongoni mwa sekta zinazolenga kuchangia katika kukuza uchumi wa Tanzania, hivyo ni muhimu kwa wadau kukutana na kujadili namna bora ya kutumia rasilimali zilizopo katika sekta hiyo.
lengo la kongamano hilo ni kuwaunganisha wadau mbalimbali ili kubadilishana uzoefu, kujadili changamoto na kutafuta suluhisho litakalowezesha uchumi wa bluu kuwa na tija zaidi kwa wananchi na taifa kwa ujumla.
“Lengo hasa la kongamano hili ni kuwakutanisha wadau wa uchumi wa bluu waweze kutafakari namna gani tunaweza kuwezesha uchumi wa bluu, ili tutoke katika kiwango tulichopo sasa na kufikia hatua ambayo inaweza kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja, lakini pia kukuza uchumi wa taifa,” amesema.
Amesema kongamano hilo pia litatoa fursa kwa watafiti kuwasilisha tafiti mbalimbali walizofanya, huku washiriki wakijadili matokeo ya tafiti hizo na kutoa maoni yatakayosaidia kuboresha shughuli zinazohusiana na uchumi wa buluu
pamoja na kukuza uchumi wa taifa, ni muhimu kuhakikisha wananchi wanapata elimu na uelewa wa kutosha kuhusu fursa zinazopatikana katika uchumi wa bluu ili waweze kuzitumia kuboresha maisha yao.
“Tunataka kuwapa Watanzania uelewa wa shughuli za uchumi wa bluu na namna wanavyoweza kufanya vizuri zaidi katika shughuli ambazo tayari wamekuwa wakizifanya kwa miaka mingi. Tukipata Watanzania wenye uelewa, elimu na ujuzi, ndipo tutakapoweza kupata ubunifu na maendeleo ya sayansi na teknolojia,” amesema Profesa Gurumo.
Chuo cha Bahari Dar es Salaam, ni taasisi ambayo imejikita katika kutoa elimu na mafunzo yanayohusiana na masuala ya bahari, kufanya tafiti na kutoa ushauri kwa Serikali pamoja na taasisi binafsi.
Katika hatua nyingine chuo hicho kinaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu uchumi wa bluu ili kuongeza uelewa wa fursa zilizopo, kuimarisha mifumo na sera, pamoja na kuwahamasisha wawekezaji kutumia fursa hizo.
Hivyo kongamano hilo litawakutanisha washiriki kutoka taasisi za serikali na binafsi, watafiti, wanataaluma, wawekezaji na wadau wa maendeleo kutoka Tanzania na mataifa mbalimbali.
Sanjari na hayo Baadhi ya nchi za Afrika ambazo zimethibitisha kushiriki ni pamoja na Comoro, Kenya, Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, huku nchi nyingine nje ya Afrika zikiwemo China, Sweden na Canada pia zikitarajiwa kushiriki.
Kupitia washiriki hao watapata fursa ya kujadili tafiti na kuonesha ubunifu mbalimbali unaohusiana na matumizi ya rasilimali za bahari na maendeleo ya uchumi wa bluu.
Aidha baada ya kukamilika kwa kongamano hilo, wanatarajia kupata maarifa mapya yatakayowanufaisha Watanzania na washiriki wengine, pamoja na mapendekezo ya kisera yatakayosaidia kuboresha mazingira ya kufanya shughuli za uchumi wa bluu.
“Tunatarajia kupata mapendekezo ya kisera. Zipo sera ambazo zinatumika, lakini kutokana na mabadiliko yanayotokea, kuna umuhimu wa kuangalia kama zinahitaji marekebisho au kama kuna maeneo yanahitaji sera mpya,” amesema Profesa Gurumo.


Social Plugin