Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

‎IOM DUNIANI NA UHAMIAJI TANZANIA WAZINDUA MFUMO WA URATIBU WA KITAIFA KUHUSU UHAMIAJI NCHINI TANZANIA


‎Na Konstebo Nangigi Mohamed, Dodoma.
‎Mfumo wa Uratibu wa Uhamiaji Kitaifa kati ya Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) Duniani na Idara ya Uhamiaji Tanzania umezinduliwa leo tarehe 18 Agosti 2026, katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Mabeyo Hall Jijini Dodoma huku ukiwa na lengo la kuimarisha ushirikiano, uratibu na ufanisi katika usimamizi wa masuala ya uhamiaji nchini, pamoja na kuimarisha diplomasia na kukuza uchumi.
‎Akizungumza katika hafla hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Mhe. Patrobas Katambi (Mb) ambaye alikuwa Mgeni Rasmi amesema Tanzania inathamini mchango na ushirikiano wa wadau mbalimbali katika kusimamia masuala ya uhamiaji, hususan IOM, ambayo ni miongoni mwa washirika muhimu.
‎“Tanzania inathamini ushirikiano na wadau mbalimbali, wakiwemo IOM, katika kuhakikisha tunaimarisha mifumo na uwezo wa kusimamia uhamiaji kwa ufanisi. Uhamiaji unajumuisha afya, maendeleo, ajira, mitaji na usalama wa kitaifa. Haya yote yafanyike bila kuathiri usalama, utu na heshima ya jamii na taifa” ,amesema Waziri Katambi.
‎Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa IOM Duniani Amy Pope, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano na mifumo madhubuti ya uratibu katika kukabiliana na changamoto za uhamiaji
‎Amesema ushirikiano kati ya IOM na Serikali ya Tanzania una nafasi kubwa katika kuimarisha usimamizi wa uhamiaji na kuhakikisha sera na mifumo iliyopo inawanufaisha wahamiaji pamoja na jamii zinazowapokea.
‎Naye Bi. Susan Namondo, Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa (UN) ameeleza kuwa uratibu wa pamoja ni muhimu katika kuhakikisha wadau wa uhamiaji wanafanya kazi kwa mwelekeo mmoja.
‎Akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Kamishna Amiru Sadick, amesema Idara ya Uhamiaji itaendelea kushirikiana na IOM na wadau wengine katika kuimarisha usimamizi wa uhamiaji salama, wenye utaratibu na unaozingatia haki za wahamiaji.
‎Kwa Upande wake Bw. Ashraf Hassan Mkuu wa Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) Tanzania  amesisitiza kuwa uhamiaji ni suala la kimataifa linalohitaji ushirikiano wa nchi na mashirika ya kimataifa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com