Na Cletus Sanga, WAF – Kibiti
Huduma za dharura nchini zimeendelea kuimarika kupitia hatua mbalimbali zinazochukuliwa na Serikali katika kuimarisha mfumo wa huduma za dharura, ikiwemo kuongeza na kuboresha magari ya wagonjwa ili kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wanaohitaji msaada wa haraka.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Afya kabla ya kumkaribisha Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa leo tarehe 08 Agosti, 2026 katika hafla ya makabidhiano ya gari la wagonjwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Kibiti, Mkoa wa Pwani, Mkurugenzi wa Huduma za Dharura na Maafa wa Wizara ya Afya, Dkt. Erasto Sylvanus, amesema kuongezeka kwa magari ya wagonjwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wagonjwa na majeruhi wanapata huduma kwa wakati na kwa usalama.
Amesema huduma za dharura zinahitaji mfumo unaofanya kazi kwa ufanisi kuanzia upatikanaji wa ambulance, vifaa muhimu, wahudumu wenye ujuzi, mawasiliano na uratibu wa rufaa, kwa kuwa katika dharura kuchelewa kwa muda mfupi kunaweza kuathiri afya na maisha ya mgonjwa.
Dkt. Sylvanus amesema tathmini ya kitaifa ya magari ya wagonjwa kwa mwaka 2025/2026 imebaini kuwa Tanzania Bara ina jumla ya magari 1,224 katika mikoa 26, hatua inayoonesha uwekezaji unaoendelea kufanywa katika huduma za dharura.
Amesema Serikali inaendelea kukamilisha mfumo wa kitaifa wa huduma za ambulance utakaoboresha uratibu wa huduma, ufuatiliaji wa magari na kuunganisha huduma hizo na namba ya dharura *115 bila malipo*, ili mwananchi anayepata dharura aweze kupata msaada unaoratibiwa, kwa wakati na kwa usalama.
Aidha, Dkt. Sylvanus amesisitiza kuwa pamoja na kuendelea kuongeza magari ya wagonjwa, ni muhimu yaliyopo kutunzwa na kufanyiwa matengenezo kwa wakati ili yaendelee kuwa tayari kutoa huduma muda wote, akieleza kuwa mafanikio ya uwekezaji huo yatapimwa kwa uwezo wa magari kufanya kazi, wagonjwa kufikiwa kwa wakati na maisha kuokolewa.




Social Plugin