
Na Elizabeth Cosmas, Malunde 1 blog - Mbogwe
SHIRIKA la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC) limeeleza kuridhishwa na maendeleo ya utekelezaji wa Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP), hususani katika Kituo Namba Nne cha kupozea mafuta ghafi kilichopo Kijiji cha Lubeho, Kata ya Nyakafuru, Halmashauri ya Mbogwe mkoani Geita.
Kituo hicho namba nne cha kupasha moto na kuongeza kasi ya mafuta kimefikia asilimia 88 ya utekelezaji na kinatarajiwa kukamilika mwezi Oktoba mwaka huu, huku mradi mzima wa bomba la mafuta ghafi unaoanzia Chongoleani mkoani Tanga hadi Hoima nchini Uganda ukiwa umefikia asilimia 90 ukitarajiwa kukamilika na kukabidhiwa mwezi Desemba mwaka 2026 na mpaka sasa Mradi mzima umetoa ajira ya zaidi ya Watanzania 11,000.
Akizungumza leo Agosti 8,2026 ,Mkurugenzi wa Mipango na Uwekezaji kutoka TPDC, Derick Moshi, amesema hayo wakati wa ziara ya kutembelea Kituo Namba Nne, akiwa ameambatana na wataalamu mbalimbali kutoka TPDC pamoja na wataalamu kutoka Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi Afrika Mashariki (EACOP).
Moshi amesema maendeleo ya utekelezaji wa kituo hicho yanaendelea vizuri huku juhudi zikiendelea kuhakikisha mradi mzima unakamilika kwa wakati uliopangwa.

“Mradi huu unatoa ajira kwa Watanzania 420. Ushirikishwaji wa jamii unaonekana, barabara zinarekebishwa na maeneo yenye changamoto za maji pamoja na zahanati yanapatiwa huduma, hivyo manufaa ya mradi yanaonekana,” amesema Moshi.
Moshi pia amesema TPDC inaendelea kufuatilia utekelezaji wa huduma za Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) katika maeneo yanayozunguka mradi huo ili kuhakikisha jamii inanufaika na uwepo wa mradi.
Aidha, Naibu Meneja wa Ulinzi wa Mradi wa EACOP Tanzania, Peter Masapa, amesema ulinzi katika maeneo ambayo bomba la mafuta ghafi linapita unaimarishwa kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kampuni binafsi za ulinzi pamoja na wananchi.
Masapa amesema Tanzania pekee ina jumla ya walinzi 1,320 wanaohusika katika ulinzi wa mradi huo, huku baadhi yao wakiendelea kupatiwa mafunzo zaidi kuhusu ulinzi na usalama.
“Tuna walinzi 1,320 kwa Tanzania pekee kwenye mradi huu ambao tayari baadhi yao wanaanza kupatiwa mafunzo zaidi juu ya ulinzi, tukianza na kundi la askari na sekta binafsi. Ulinzi upo wa kutosha na unaendelea kuimarika zaidi,” amesema Masapa.
Msimamizi wa Maudhui ya Ndani (Local Content) kutoka EACOP, Neema Kweka, amesema lengo la ziara hiyo ni kuiwezesha Serikali kufuatilia utekelezaji wa mipango iliyowekwa kwa pamoja, hususani kuhakikisha maudhui ya ndani yanatekelezwa ipasavyo katika jamii.
Kweka amesema utekelezaji wa maudhui ya ndani unazingatia matakwa ya sheria ya mwaka 2017, huku utoaji wa ajira kwa wazawa katika mradi huo ukifikia zaidi ya asilimia 82.
Naye Mkurugenzi wa Rasilimali Watu na Mahusiano ya Kampuni kutoka EACOP, Geofrey Mponda, amesema jamii zinazozunguka mradi huo zinaendelea kupata manufaa mbalimbali kupitia utekelezaji wa shughuli za kijamii.
Mponda amesema zaidi ya wanafunzi 4,000 nchini wananufaika na mradi huo kupitia upatikanaji wa vifaa mbalimbali vya kujifunzia, huku wakulima nao wakiwezeshwa pembejeo za kilimo kwa lengo la kuongeza uzalishaji na kuinua kipato.
Hata hivyo baadhi ya vijana walioajiriwa katika mradi huo kupitia Kituo Namba Nne kilichopo Kijiji cha Lubeho, akiwemo Paul Chasama na Eustace Majura, wamesema ajira hizo zinawapa fursa ya kupata kipato huku zikiwawezesha kujifunza na kuongeza ujuzi wa kitaalamu.
Vijana hao wamebainisha kuwa tangu wamejiunga katika mradi huo mwaka 2024 wakiwa hawana ujuzi wa ufundi wamepata ujuzi mpya huku wakitumia mafunzo na uzoefu walioupata kujitegemea kiuchumi.
Wamesema uzoefu walioupata kupitia mradi huo umewajengea uwezo wa kujiajiri na kutumia ujuzi huo katika shughuli nyingine za kiuchumi hata baada ya mradi kukamilika.








Social Plugin