Na. Mwandishi Wetu ,Kazuramimba Kigoma
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Dkt. Jim Yonazi, Amewaasa vijana kulinda afya zao na kuepuka tabia hatarishi ili kupunguza maambukizi mapya ya VVU, kwa kuzingatia kuwa ni kundi linaloongoza kuwa hatarini zaidi nchini Tanzania.
Dkt. Yonazi ameyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa Afua za UKIMWI Wilaya ya Uvinza Mkoa wa Kigoma alipoambatana na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania, Dkt. Adam Mrisho, timu ya wataalam kutoka Ofisi yake, Wizara ya Afya, TAMISEMI na Ofisi ya Mkoa huo.
Aidha amepata wasaa kutembelea Kituo cha Maarifa Kata ya Kazuramimba mkoani humo kinachotoa huduma za masuala ya VVU na UKIMWI, na kukutana na vijana wanaotekeleza afua za UKIMWI kupitia vikundi vya uzalishaji mali kwa lengo la kujiinua kiuchumi na kujiletea maendeleo yao.
Akiwa katika kituo hicho, Dkt. Yonazi amepokea taarifa kutoka kwa mwenyekiti wa kikundi, Billy Sekibaha, kuhusu shughuli zinazofanywa na kikundi hicho ikiwemo za biashara ndogondogo za kuuza dagaa pamoja na shunguli za ushonaji wa nguo kwa lengo la kujikwamua kiuchumi na kuondokana na dhana ya utegemezi.
Amesisitiza kuwa, kundi la vijana linategemewa na Taifa katika shughuli za uzalishaji mali na kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla hivyo ni vyema vijana wakaendelea kujilinda na kulinda wengine kwa kutambua hali zao na endapo wakagundulika kuwa na maambukizi ya VVU inashauriwa kuanza kutumia dawa mapema.
"Mnafanya kazi nzuri sana, endeleeni kuchangamkia uwepo wa mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa zenu ili kuwafikia wateja wengi zaidi na kujitangaza kitaifa na kimataifa," alisisitiza Dkt. Yonazi
Kwa upande wake Mtendaji wa TACAIDS, Dkt. Adam Mrisho amewapongeza vijana hao kwa kazi nzuri wanazofanya na kusisitiza kuwa Tume itaendelea kuwawezesha vijana kiuchumi na kuwajengea uwezo ili kuendeleza mapambano dhidi ya maambukizi mapya ya VVU na kufikia lengo la kutokomeza UKIMWI ifikapo mwaka 2030.







Social Plugin