
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya uteuzi na uhamisho wa Wakuu wa Mkoa na Makatibu Tawala wa Mkoa, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo tarehe 27 Agosti 2026 na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dkt. Moses Kusiluka.
Katika uteuzi huo wa Wakuu wa Mkoa, CP. Salum Rashid Hamduni aliyekuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Bw. Alexander Pastory Mnyeti ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Bw. Stanslaus Haron Nyongo ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Pwani, na Bw. Jumanne Abdallah Sagini ameteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya.
Aidha, Wakuu wa Mkoa waliohamishwa ni pamoja na Mhe. Martine Reuben Shigela aliyetoka Mkoa wa Geita kwenda Manyara, Mhe. Said Mohamed Mtanda aliyetoka Mwanza kwenda Simiyu kuchukua nafasi ya Bw. Anamringi Macha aliyestaafu, Mhe. Abubakar Mussa Kunenge aliyetoka Pwani kwenda Songwe kuchukua nafasi ya Bw. Jabiri Omari Makame ambaye atapangiwa majukumu mengine, na Mhe. Beno Moris Malisa aliyetoka Mbeya kwenda Tabora kuchukua nafasi ya Bw. Paul Matiko Chacha ambaye ameteuliwa kuwa Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) - Idara ya Organizesheni.
Wengine ni Mhe. Adam Kighoma Malima aliyetoka Morogoro kwenda Lindi kuchukua nafasi ya Bi. Zainab Telack aliyestaafu, na Mhe. Queen Cuthbert Sendiga aliyetoka Manyara kwenda Morogoro.
Katika upande wa Makatibu Tawala wa Mkoa, Bw. Richard Marcellino Kayombo ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani. Waliouhamishwa katika nafasi hiyo ni pamoja na Bw. Balandya Mayuganya Elikana kutoka Mwanza kwenda Mbeya, Dkt. Fatuma Ramadhan Mganga kutoka Singida kwenda Mwanza, Bi. Pili Hassan Mnyema kutoka Pwani kwenda Shinyanga, na Bw. Rodrick Lazaro Mpogolo kutoka Mbeya kwenda Singida. Taarifa hiyo imefafanua kuwa tarehe ya uapisho wa viongozi hao wote wateule itapangwa baadaye.



Social Plugin