
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Emmanuel John Nchimbi, ametangaza kujiuzulu nafasi hiyo kuanzia Septemba 4, 2026, huku akieleza pia kuwa ameamua kustaafu siasa na utumishi wa umma.
Dkt. Nchimbi ametoa taarifa hiyo leo Jumanne, Agosti 25, 2026, akisema amemwandikia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kumjulisha kuhusu uamuzi wake.
Katika taarifa yake, Dkt. Nchimbi amesema uamuzi huo umefikiwa kwa kuzingatia Ibara ya 50(2)(c) ikisomwa pamoja na Ibara ya 149(2) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema uamuzi huo unatekeleza ahadi aliyompa Rais Samia Agosti 27, 2025, kwamba angemsaidia Rais na nchi kwa uwezo wake wote na kwa uaminifu, huku akiahidi kuachia nafasi hiyo endapo Rais angeona kuna haja ya kuwa na Makamu mwingine wa Rais.
“Nimejiridhisha pasipo shaka kuwa Mhe. Rais anatamani mabadiliko, hivyo nimeamua kutimiza ahadi yangu,” amesema Dkt. Nchimbi katika taarifa hiyo.

Dkt. Nchimbi pia amemshukuru Rais Samia na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa imani waliyoonyesha kwake, pamoja na Watanzania kwa ushirikiano waliompa katika kipindi chote cha utumishi wake wa umma.
Amesema licha ya kustaafu siasa na utumishi wa umma, ataendelea kuwa raia mwema wa Tanzania.
Dkt. Nchimbi aliteuliwa kuwa Makamu wa Rais tarehe 27 Agosti 2025 na baadaye kuapishwa kushika wadhifa huo Novemba 3, 2025.
Social Plugin