
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) imeteketeza hekari 3,117.9 za mashamba ya bangi na kukamata watuhumiwa 12 katika operesheni maalum ya siku 16 iliyofanyika katika vijiji vinne vya Kata ya Kandawale na Kipatimo, Wilaya ya Kilwa, mkoani Lindi.
Akizungumza kuhusu operesheni hiyo, Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa kati ya Mamlaka, wananchi na viongozi wa maeneo husika katika mapambano dhidi ya kilimo cha bangi.
Amesema operesheni hiyo ni sehemu ya mkakati endelevu wa DCEA wa kudhibiti uzalishaji wa dawa za kulevya nchini hususan bangi, ambayo imeendelea kulimwa katika baadhi ya maeneo nchini.
"Tumebaini uwepo wa mashamba makubwa ya bangi yaliyolimwa katika ardhi zinazomilikiwa na vijiji na vitongoji. Licha ya serikali kuweka mkakati wa matumizi ya ardhi iliyopo chini ya vijiji na vitongoji lakini bado wananchi wanaitumia ardhi hiyo kulima bangi" amesema Lyimo.
Ameeleza kuwa, kati ya wananchi 200 hadi 250 walishiriki kila siku katika kufyeka mashamba hayo, jambo linalodhihirisha umuhimu wa ushiriki wa jamii katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi wote wenye mashamba ya bangi au wanaofahamu uwepo wa mashamba hayo katika maeneo yao nchini kuyateketeza mara moja kabla ya hatua za kisheria kuchukuliwa. Vilevile, amewataka viongozi wa vijiji na kata kuhakikisha wanazuia na kutokomeza kilimo cha bangi katika maeneo yao.
Vilevile, amewataka wasimamizi wa hifadhi za taifa na maeneo mengine ya uhifadhi kuhakikisha maeneo wanayosimamia hayatumiki kulima bangi, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya yeyote atakayebainika kuruhusu au kushindwa kudhibiti shughuli hizo.
Kwa upande wao, wananchi wa Kijiji cha Nandete, Veronica Mandai na Nassoro Mbonde, wamelaani vikali uwepo wa kilimo cha bangi katika maeneo yao, wakisema kuwa hakina manufaa kwa jamii na kimekuwa kikihatarisha mustakabali wa vijana.
Wamesema wakati mwingine watoto wao hujihusisha na kilimo hicho bila wazazi kufahamu, ndiyo sababu wamejitokeza kwa wingi kushiriki katika zoezi la kuteketeza mashamba ya bangi ili kuonyesha msimamo wao wa kupinga kilimo hicho.
"Nawaomba vijana na wanawake wawe mstari wa mbele kukataa na kutokomeza dawa za kulevya kwa sababu zina madhara makubwa kwa afya na maendeleo ya jamii. Vijana ndiyo nguvu kazi ya taifa na wanawajibu wa kulijenga Taifa. Wakijiingiza katika matumizi au uzalishaji wa dawa za kulevya, watapoteza fursa hiyo na kuathiri maendeleo ya taifa. Vilevile, watoto wanaokulia katika mazingira yanayohusisha dawa za kulevya wako katika hatari ya kupoteza mwelekeo wa maisha yao," amesema Veronica.
Naye Afisa Mtendaji wa Kata ya Kandawale, Mohamed Mpame, amesema baada ya operesheni hiyo viongozi wa kata kwa kushirikiana na vijiji na vitongoji wataimarisha ulinzi na usimamizi wa maeneo yao ili kuhakikisha kilimo cha bangi hakiendelei.
"Tutahakikisha tunafanya doria za mara kwa mara na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili waachane kabisa na kilimo cha bangi ili mwisho wa siku likitokea la kutokea iwe ni juu yao. Nawashauri watu kutumia ardhi yao kulima mazao ya korosho na kuachana na mazao ya bangi” amesema Mpame.
DCEA itaendelea kufanya operesheni nchi nzima kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali ili kubaini na kutokomeza maeneo yote yanayotumika kwa kilimo cha bangi na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa mujibu wa sheria.

















Social Plugin