Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WIKI YA KITAIFA YA ELIMU, UJUZI NA UBUNIFU KUFANYIKA TANGA, ZAIDI YA BUNIFU 70 KUPEWA MSUKUMO WA KIBIASHARA










Na Mwandishi Maalum

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, ametangaza kuwa Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu kwa mwaka 2026 yatafanyika kuanzia Agosti 15 hadi 24 katika Viwanja vya Michezo vya Shule ya Sekondari Usagara, jijini Tanga, yakilenga kuonesha mafanikio ya sekta ya elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu nchini.

Akizungumza jijini Dar Es Salaam Prof. Mkenda amesema wiki hiyo itawakutanisha wadau kutoka wizara mbalimbali, vyuo vya elimu ya juu, vyuo vya ufundi na ufundi stadi, taasisi za utafiti pamoja na sekta binafsi kwa ajili ya maonesho, mijadala ya kimkakati na kubadilishana uzoefu kuhusu maendeleo ya elimu, ujuzi na ubunifu.

Amesema wananchi watapata fursa ya kushuhudia bunifu mbalimbali zilizobuniwa na vijana wa Kitanzania, zikiwemo ambazo tayari zimeingia sokoni pamoja na zile zinazokamilishwa kwa ajili ya matumizi ya kibiashara.

Miongoni mwa bunifu zitakazooneshwa ni mashine ya kukamua mafuta ya parachichi (Avomero), mabegi ya shule yenye mfumo wa nishati ya jua (Soma Bags) na mita janja za maji (Smart Prepaid Water Meter).





Prof. Mkenda amesema bunifu hizo ni uthibitisho wa mafanikio ya jitihada za Serikali katika kuwawezesha wabunifu wa ndani na kuendeleza bidhaa zinazotoa suluhisho kwa changamoto za kijamii na kiuchumi.

Ameongeza kuwa kwa sasa zaidi ya bunifu 70 zipo katika hatua mbalimbali za kukuzwa ili ziwe biashara halisi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

"Serikali imeanzisha mfuko maalum wa kuwasaidia wabunifu ili kupunguza gharama za uzalishaji na kuharakisha ukuaji wa biashara zao," amesema.

Prof. Mkenda pia amesema maadhimisho hayo yatahusisha Mashindano ya Kitaifa ya Ujuzi, ambayo yatafanyika kwa viwango vinavyokidhi ushindani wa kimataifa, ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya Tanzania kushiriki Mashindano ya Dunia ya Ujuzi (WorldSkills Competition).

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo, amesema Serikali ipo katika hatua za kuhuisha Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ili iendane na mabadiliko ya dunia pamoja na mahitaji ya sasa.

Amesema sera hiyo mpya itatoa mwongozo wa kitaifa kuhusu maendeleo ya sayansi, teknolojia na ubunifu, ikiwemo uratibu wa mashindano ya kitaifa ya ubunifu.


Naye Mkurugenzi wa Idara ya Sayansi, Teknolojia na Ubunifu, Prof. Ladislus Mnyone, amesema Serikali imekamilisha mkakati wa kuongeza ushiriki wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi (diaspora) katika kuendeleza bunifu na teknolojia za ndani.

Amesema hadi sasa halmashauri 90 zimeanzisha madawati ya sayansi na ubunifu, hatua inayowawezesha wabunifu kuwasilisha mawazo yao na kuunganishwa na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) kwa ajili ya kuyakuza na kuyaendeleza.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), Dkt. Amos Nungu, amepongeza juhudi za Serikali katika kuhamasisha ubunifu nchini.

Amesema COSTECH itaandaa banda maalum katika maonesho hayo litakaloonesha bunifu zilizofanikiwa kuingia sokoni ili kutoa ushuhuda wa mafanikio ya wabunifu wa Kitanzania na kuhamasisha wengine kuendeleza mawazo yao.

Dkt. Nungu amesisitiza kuwa ushirikiano kati ya Serikali, taasisi mbalimbali na wananchi ni nguzo muhimu katika kuimarisha ubunifu, kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani na kuchochea maendeleo ya taifa.

Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Wiki ya Kitaifa ya Elimu, Ujuzi na Ubunifu 2026 ni: "Elimu, Ujuzi na Ubunifu: Njia ya Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050."

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com