Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAAJIRI TABORA WATAKIWA KUMALIZA CHANGAMOTO ZA WATUMISHI MWAKA HUU WA FEDHA


Na Veronica Mwafisi ,Tabora

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Ridhiwani Kikwete, amewaelekeza waajiri wote wa Sekta ya Umma mkoani Tabora kuhakikisha wanatatua changamoto zote za kiutumishi zinazowakabili watumishi ndani ya mwaka huu wa fedha ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Akizungumza July 11,2026 katika kikao cha majumuisho na viongozi pamoja na watumishi wa umma wa Mkoa wa Tabora baada ya kuhitimisha ziara yake ya kikazi ya siku tatu, Mhe. Kikwete alisema waajiri wanapaswa kushughulikia madai yote ya msingi ya watumishi, yakiwemo kupandishwa madaraja, kubadilishiwa kada wanaostahili, kulipwa malimbikizo na kutekelezewa stahiki nyingine kwa wakati.

Alisema Ofisi ya Rais imekuwa ikipokea malalamiko mengi kutoka kwa watumishi kuhusu kucheleweshwa kwa haki zao, hali ambayo imekuwa ikipunguza ari ya kazi na kuathiri ubora wa huduma zinazotolewa kwa wananchi.

"Rais wetu mpendwa, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka wananchi wapate huduma bora. Mwaka huu wa fedha tushughulikie changamoto zote za watumishi ili watoe huduma kwa furaha," alisema Mhe. Kikwete.

Aliongeza kuwa watumishi wote wanaokidhi vigezo vya kupandishwa madaraja, kubadilishiwa kada au kulipwa madai yao wanapaswa kutekelezewa bila kuchelewa. Aidha, aliwataka waajiri kufikisha ofisini kwake changamoto zozote zitakazojitokeza ili zipatiwe ufumbuzi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Kikwete aliwataka Maafisa Rasilimaliwatu kutumia taaluma zao ipasavyo kwa kuwashauri waajiri namna bora ya kushughulikia masuala ya kiutumishi.

Alisisitiza kuwa endapo changamoto za watumishi zitaendelea kuwepo bila ufumbuzi, Maafisa Rasilimaliwatu watawajibika kwa kuwa wao ndiyo washauri wakuu wa waajiri katika masuala ya utumishi.

Waziri huyo pia aliwapongeza viongozi na watumishi wa Mkoa wa Tabora kwa ushirikiano mzuri uliopo kati ya Serikali na Chama Cha Mapinduzi (CCM), akisema umesaidia kuharakisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo na huduma kwa wananchi.

"Tunatekeleza Ilani ya Chama kilichoko madarakani. Nawapongeza kwa ushirikiano baina yenu, na muendelee kufanya kazi kwa pamoja kwani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa letu," alisema.

Aidha, aliwataka viongozi na watumishi kuwa karibu zaidi na wananchi, hususan vijana, kwa kusikiliza changamoto zao na kuwasaidia kupata suluhisho badala ya kusubiri viongozi kutoka maeneo mengine kufanya kazi hiyo.

Alisema kusikiliza mahitaji ya vijana kunaweza kuwasaidia kupata fursa za kujikwamua kiuchumi na kuwaepusha kujiingiza katika vitendo visivyo na maadili.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Tabora, Bi. Upendo Wella, alimshukuru Mhe. Ridhiwani Kikwete kwa kufanya ziara hiyo, akisema imeongeza hamasa kwa watumishi na itachangia kuboresha utendaji kazi pamoja na maendeleo ya Mkoa wa Tabora na Taifa kwa ujumla.








Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com