Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TANZANIA YAITAKA WIPO KUJENGA MFUMO JUMUISHI WA MILIKI BUNIFU ILI NCHI ZINAZOENDELEA ZINUFAIKE NA AKILI UNDE

    


Geneva, Julai 2026 

Tanzania imelitaka Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) kujenga mfumo wa kimataifa wa miliki bunifu unaowezesha nchi zinazoendelea kunufaika na maendeleo ya akili unde (Artificial Intelligence–AI), huku ikisisitiza umuhimu wa kuhamasisha matumizi ya teknolojia na kujengea watu uwezo.

Akiwasilisha taarifa ya nchi kwa niaba ya Mhe Balozi Possi katika Mkutano wa 68 wa Nchi Wanachama wa Shirika la Miliki Ubunifu Duniani (WIPO) ulioanza tarehe 7 Julai, 2026 na kufanyika Geneva Uswisi, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Hoyce Temu, alisema miliki ubunifu imekuwa nyenzo muhimu ya kukuza ubunifu, viwanda na maendeleo ya uchumi.

"Tanzania inatambua miliki ubunifu kama kichocheo cha kimkakati cha ubunifu, uvumbuzi wa teknolojia, maendeleo ya viwanda na maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi," alisema.

Alisema Tanzania inaendelea kujenga uchumi unaotegemea maarifa na inaiona akili mnemba kama fursa ya kuongeza kasi ya ubunifu na ukuaji wa uchumi.

"Tunaamini kuwa mifumo jumuishi ya miliki bunifu, ujenzi wa uwezo na uhamishaji wa teknolojia ni muhimu ili kuwezesha nchi zinazoendelea kunufaika kikamilifu na akili mnemba pamoja na teknolojia nyingine zinazoibuka," alisema.

Kauli hiyo inakuja wakati mataifa duniani yanaendelea kujadili namna mfumo wa miliki ubunifu utakavyoweza kuendana na kasi ya maendeleo ya akili mnemba. Nchi nyingi zinazoendelea zimekuwa zikitaka ushirikiano mkubwa zaidi katika uhamishaji wa teknolojia na maarifa ili kupunguza pengo la kidijitali.

Balozi Temu alisema Tanzania inaendelea kuimarisha mfumo wake wa miliki bunifu kupitia mageuzi ya sheria, kuboresha utoaji wa huduma, kuimarisha utekelezaji wa sheria, kujenga uwezo wa taasisi na kuongeza uelewa wa umma.

Aliishukuru WIPO kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania kupitia programu mbalimbali za kiufundi na ujenzi wa uwezo, ikiwemo kliniki za usimamizi wa haki miliki kwa biashara ndogo na za kati pamoja na kampuni changa, miradi ya uhamishaji wa teknolojia kupitia vyuo vikuu na taasisi za utafiti, mafunzo ya uchunguzi wa hataza na uwekaji wa mfumo wa kidijitali wa usimamizi wa haki miliki.

"Tunaendelea kujizatiti kuimarisha mfumo wa haki miliki ili uchangie zaidi katika ubunifu, uwekezaji, ujasiriamali, ajira na ukuaji endelevu wa uchumi," alisema.

Balozi Temu alisisitiza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na WIPO pamoja na nchi nyingine wanachama kujenga mfumo wa haki miliki unaojumuisha wote, unaozingatia usawa na unaoweza kukidhi mahitaji ya teknolojia za sasa na zijazo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com