Balozi wa Uingereza nchini, Mhe. Marianne Young amefanya mazungumzo na Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Bi. Ellen Maduhu, katika Ofisi Ndogo za Wizara jijini Dar es Salaam tarehe 30 Julai 2026.Mazungumzo hayo yalikuwa ya kwanza kufanyika kati ya viongozi hao wawili tangu Bi. Maduhu aanze kutekeleza majukumu yake kama Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ulaya na Marekani. Mazungumzo hayo yalitoa fursa ya kuimarisha mahusiano ya kikazi na kubadilishana mawazo kuhusu masuala mbalimbali ya ushirikiano.
Katika mazungumzo hayo, pande zote mbili zilikubaliana kuendeleza na kuimarisha ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Tanzania na Uingereza, sambamba na kutafuta fursa mpya za ushirikiano katika maeneo yenye maslahi ya pamoja kwa manufaa ya nchi hizo mbili.
Viongozi hao walisisitiza umuhimu wa kuendelea kushirikiana kwa karibu katika nyanja za uchumi, biashara na uwekezaji, maendeleo ya kijamii pamoja na masuala ya kidiplomasia, kwa lengo la kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki na kuleta manufaa kwa wananchi wa Tanzania na Uingereza.
Social Plugin