Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SGR MAKUTOPORA-TABORA KURAHISISHA BIASHARA KANDA YA KATI,MAGHARIBI



Na Sheila Ahmadi, Tabora

Mkoa wa Tabora unatarajiwa kuwa kitovu muhimu cha usafiri wa reli nchini baada ya kukamilika kwa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) wa Makutopora–Tabora, ambapo kituo kikuu kitakachounganisha njia za reli kuelekea Mwanza na Kigoma kitajengwa.

Hayo yamesemwa na Meneja wa mradi huo, Mhandisi Christopher Kalisti, amesema kuwa ujenzi wa kipande hicho unaendelea kwa mujibu wa ratiba naunatarajiwa kukamilika mwaka 2028.

" Mradi huo unahusisha ujenzi wa kilomita 294 za njia kuu ya reli pamoja na kilomita 74 za njia za michepuko zitakazorahisisha usafiri na kuunganisha maeneo ya uzalishaji na biashara.

Akizungumza Julai 18 Mwaka huu 2026 katika eneo la Nyahua, mkoani tabora Kalisti amesema mbali na kituo kikuu cha Tabora, vituo vya abiria na mizigo vitajengwa Manyoni na Itigi, huku Goweko na Igalula vikijengewa vituo vya kuhudumia wananchi na wafanyabiashara.

Aidha kukamilika kwa reli hiyo kutarahisisha usafirishaji wa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Kanda ya Kati, Magharibi pamoja na nchi jirani, hatua itakayoongeza ufanisi wa biashara na kupunguza gharama za usafirishaji.

Kalisti ameongeza kuwa reli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba tani 35 kwa kila ekseli, jambo litakalopunguza muda wa safari kati ya Dar es Salaam, Dodoma na Tabora na kuongeza uwezo wa kusafirisha mizigo kwa ufanisi.

Kwa upande wake, Mhandisi Pangapanga Msisili wa kampuni ya Yapi Markezi amesema kazi za ujenzi zinaendelea kwa kiwango kinachoridhisha na hazijawahi kusimama tangu zilipoanza.

Vilevile mkandarasi ameendelea kuzingatia ratiba ya utekelezaji ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kuanza kutoa huduma zitakazochochea ukuaji wa uchumi na kuimarisha sekta ya usafiri nchini.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com