Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAFANYA MABORESHO YA DAFTARI LA ARDHI VIJIJI VYA NGORONGORO, YAFAFANUA NOTISI ZA UBORESHWAJI




Na Mwandishi wetu,Dodoma

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imefafanua kuhusu notisi zilizotolewa kwa wananchi wa vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Enguserosambu, Arash na Losoito vilivyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, ikieleza kuwa hatua hiyo inalenga kuboresha taarifa za usajili wa ardhi na kuondoa changamoto za kumbukumbu za umiliki.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara hiyo, notisi hizo zilitolewa tarehe 4 Juni, 2026 na Ofisi ya Msajili wa Hati Mkoa wa Arusha kwa vijiji hivyo kwa lengo la kurekebisha Daftari la Msajili ili kuondoa kumbukumbu za usajili wa hati miliki zilizotolewa kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura ya 114.

Wizara imeeleza kuwa utaratibu huo unahusisha kurekebisha Daftari la Kumbukumbu za Usajili kwa kuondoa hatimiliki na kutoa Cheti cha Ardhi ya Kijiji kinachotambua mamlaka ya halmashauri za vijiji hivyo kusimamia ardhi kwa ajili ya wananchi wake kwa mujibu wa sheria.

“Utaratibu huu umekuwa ukitumika katika vijiji vingine nchini vilivyokuwa na hali kama hiyo kabla ya kuanza kutumika kwa Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura ya 114,” imeeleza taarifa hiyo.

Aidha, Wizara imefafanua kuwa baada ya kukamilika kwa mchakato huo, vijiji vya Ololosokwan, Soitsambu, Enguserosambu, Arash na Losoito vitabaki kuwa na nyaraka rasmi ya Cheti cha Ardhi ya Kijiji, ambayo ndiyo itakayotumika kama msingi wa usimamizi wa ardhi kwa manufaa ya wanakijiji kwa mujibu wa sheria.

Wizara imewataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai kuwa kuna mpango wa kuchukua ardhi za vijiji hivyo na kuzipeleka kwenye matumizi mengine, ikisisitiza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya maboresho ya kiutawala ya taarifa za ardhi.

“Wizara inawatakia wananchi kupuuza upotoshaji wowote unaotolewa kuhusiana na mchakato huu kwamba unanuiwa kuchukua ardhi za vijiji tajwa na kuzipeleka kwenye mamlaka nyingine ya usimamizi, mwekezaji au mwananchi yeyote,” imeeleza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo imetolewa na Eleuteri Mangi, Mkurugenzi wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com