Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI INATHAMINI MCHANGO WA TAASISI ZA DINI




Na Mwandishi - Karagwe.


WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano Mhe. Deus Sangu amesema Serikali itaendelea kudumisha ushirikiano na taasisi za dini katika kuimarisha amani, umoja, maadili na maendeleo ya Taifa.

Amesema hayo leo Julai 26, 2026 wakati alipomwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba katika Harambee ya ujenzi wa Dayosisi ya Karagwe Mkoani Kagera.

Amesema, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatambua na kuthamini mchango mkubwa wa taasisi za dini katika ujenzi wa Taifa. Makanisa yamekuwa washirika muhimu katika kutoa huduma za elimu, afya, malezi ya vijana, kusaidia wahitaji na kujenga jamii yenye maadili mema.


Kwa upande mwengine, Waziri Sangu amesema taasisi za dini zimeendelea kutekeleza jukumu kubwa la kujenga jamii yenye maadili kupitia mafundisho yanayotolewa kwenye mimbari na madhabahu, hivyo amesisitiza viongozi wa dini Kuimarisha umoja na mshikamano wa kijamii; Kukuza maadili ya uadilifu, uwajibikaji, uaminifu na upendo katika jamii.

Pia, amehimiza elimu ya malezi bora kwa wazazi, vijana na watoto kutolewa, Kuelimisha wananchi kuhusu umuhimu wa amani, umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na Kuhimiza kuheshimiana, kuvumiliana, kupendana na kuishi kwa ustahimilivu katika jamii.

“Tukisimamia mambo hayo tutaendelea kujenga Taifa lenye umoja, amani na mshikamano, ambalo ni msingi wa ustawi wa wananchi na maendeleo ya Tanzania” amesema


Katika harambee hiyo Mheshimiwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Nchemba amechangia kiasi cha Shilingi 30,000,0000/= kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa majengo ya Kanisa hilo. Vilevile, Waziri Sangu ameunga mkono jitihada hizo kwa kutoa Shilingi 5,000,000/=.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Kanali Yahya Ramadhan, amesema ujenzi wa nyumba za ibada ni uwekezaji mkubwa wa kiroho, maadili na malezi ya jamii. Ameongeza kuwa kukamilika kwa Kanisa hilo kutapelekea Jimbo Teule la Nkwenda kuwa Jimbo kamili, na hivyo waumini kupata huduma za kiroho kwa ukaribu zaidi.

Kwa upande wake, Mchungaji Jeremiah Rugimbana, Katibu Mkuu wa KKKT Jimbo Teule la Nkwenda, ameishukuru Serikali kwa kuthamini mchango wa taasisi za dini na kushiriki moja kwa moja katika maendeleo ya kijamii, ikiwemo kukamilisha ujenzi wa Kanisa hilo.

Ameongeza kuwa, ushirikiano huu ni kielelezo cha mshikamano wa kitaifa na dhamira ya Serikali ya kujenga jamii yenye maadili thabiti na mshikamano wa kudumu.







Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com