Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

ASKARI WA WANYAPORI BABATI WAPATA MAFUNZO YA HUDUMA ZA KWANZA NA ULINZI KUTOKA JESHI LA MAREKANI


Na Mwandishi Wetu, Babati

Askari 49 wa wanyamapori kutoka Hifadhi ya Jamii ya Wanyamapori Burunge (Burunge WMA), Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara, wamehitimu mafunzo ya siku nne yaliyolenga kuwaongezea uwezo wa kutoa huduma ya kwanza kwa watalii pamoja na kutumia mbinu za kisasa katika doria za kupambana na ujangili.

Mafunzo hayo yametolewa na askari wa Jeshi la Anga la Marekani kupitia Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania, kwa uratibu wa Chem Chem Association, taasisi inayojihusisha na uhifadhi na uwekezaji katika shughuli za utalii katika eneo la Burunge.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, January Bikubwa, alisema mafunzo hayo yameongeza uwezo wa askari hao katika kuhudumia watalii, kulinda rasilimali za wanyamapori na kutoa huduma kwa wananchi wanaoishi jirani na hifadhi hiyo.

"Askari hawa sasa wana ujuzi zaidi wa kutoa huduma ya kwanza kwa watalii na wananchi, sambamba na kuimarisha usalama wa hifadhi kupitia mbinu bora za doria," alisema Bikubwa.

Kwa upande wake, Afisa Wanyamapori wa Wilaya ya Babati, Beatrice Onesmo, alisema washiriki wamepatiwa mbinu za kisasa za kufanya doria ambazo zitasaidia kuongeza ufanisi katika mapambano dhidi ya ujangili.

"Askari hawa sasa wana mbinu za kisasa za kufanya doria na hivyo kuongeza uwezo wa kukabiliana na vitendo vya ujangili," alisema.

Mmoja wa wakufunzi kutoka Jeshi la Anga la Marekani, Captain Benjamin McCall, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea askari uwezo wa kutoa huduma ya kwanza kwa haraka wakati wa dharura, pamoja na kuboresha mbinu za ulinzi wa hifadhi.

"Tunaamini uwezo wao wa kutoa huduma ya kwanza umeimarika, lakini pia wameongeza uwezo wa kukabiliana na ujangili kwa kutumia mbinu za kisasa," alisema Captain McCall.

Naye Mtendaji Mkuu wa Chem Chem Association, Clever Zulu, alisema taasisi hiyo imeendelea kuratibu mafunzo hayo ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuboresha usimamizi wa hifadhi na kuifanya Burunge WMA kuwa miongoni mwa maeneo bora ya utalii barani Afrika.

Alisema lengo ni kuhakikisha hifadhi hiyo inakuwa salama, yenye wanyamapori wengi na huduma bora kwa watalii, jambo litakaloongeza idadi ya watalii wa hadhi ya juu na kuongeza mapato yatokanayo na sekta ya utalii.

"Mafunzo haya yataongeza usalama wa hifadhi na kuvutia watalii wengi zaidi, hali itakayochangia ukuaji wa mapato ya Serikali kupitia sekta ya utalii," alisema Zulu.

Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Fatuma Seleman, alisema maarifa aliyopata yatamsaidia kuboresha utendaji wake wa kila siku katika kulinda hifadhi na kuwahudumia watalii kwa ufanisi zaidi.

Mafunzo hayo ni sehemu ya programu endelevu ya kujenga uwezo wa askari wa Burunge WMA. 

Hapo awali, askari hao walipatiwa mafunzo ya matumizi ya teknolojia za kisasa katika ulinzi wa hifadhi, ukamataji wa watuhumiwa, upelelezi na uandaaji wa mashitaka, ikiwa ni jitihada za kuimarisha uhifadhi wa wanyamapori na kukuza utalii endelevu nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com