
Umoja, amani na mshikamano wa Tanzania unazidi kuimarika kupitia misingi thabiti ya utawala wa sheria na utetezi wa maslahi ya wananchi, nguvu inayochagizwa na ushirikiano wa dhati kati ya viongozi wa nchi, nguvu ya umma, na weledi wa wataalamu wa sheria.
Akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Mawakili wa Serikali mnamo Julai 13, 2026, katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, amesisitiza kuwa chama hicho kinapaswa kuwa nguzo kuu ya kulinda utulivu wa nchi na si chanzo cha migongano wala migawanyiko.
Rais alisema kuwa Watanzania wana matarajio makubwa kutoka kwa mawakili na kuwataka kutekeleze majukumu yao kwa uzalendo wa hali ya juu, uadilifu, na kulinda maslahi ya taifa dhidi ya nguvu mbalimbali za kimataifa zinazotafuta kutimiza ajenda zao binafsi kupitia mataifa mengine.
Katika kuonyesha umuhimu wa kuzuia migogoro kabla haijatokea, Rais Samia amebainisha kuwa kalamu ya Mwanasheria wa Serikali ni nyenzo yenye nguvu kubwa inayoweza kuokoa rasilimali za umma na kuzuia hasara kubwa kwa serikali kabla hazijafika, tofauti na kalamu ya Rais inayohusika katika hatua za mwisho za utekelezaji.
Ili kuhakikisha kalamu hizo zinalinda rasilimali na uhuru wa nchi, serikali imejijipanga kuendelea kuwajengea mawakili uwezo wa kitaaluma na kuboresha mazingira yao ya kazi, ambapo Rais amemwagiza Waziri wa Katiba na Sheria, Dkt. Juma Homera, kutatua changamoto zao zikiwemo zile zilizofunguliwa njia tayari kama upatikanaji wa ofisi na viwanja katika miji ya Dodoma na Arusha.
Amesema mazingira wezeshi yatawezesha sekta ya sheria kuwa chombo chenye nidhamu, maadili, na ubunifu kwa maslahi ya nchi.
Rais alisisitiza kuwa nguvu ya kisheria inaenda sambamba na jitihada za kuwafikia wananchi moja kwa moja ili kuwapa uwezo wa kujua haki zao, jambo ambalo mawakili wa serikali wamekuwa wakilifanya kupitia kliniki za sheria na utafsiri wa sheria mbalimbali kwenda kwenye lugha ya Kiswahili ili kukuza utawala wa sheria kuanzia ngazi ya chini.
'Hatua hizi ni sehemu ya maandalizi ya kufanikisha utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050, inayolenga kujenga sheria bora, mikataba imara, na taasisi zinazowajibika ili kuvutia uwekezaji na kuchangia ukuaji wa uchumi shindani na jumuishi. Kupitia mifumo hii, taifa linasimamia maendeleo ya kweli yanayohakikisha kuwa hakuna mwananchi anayeachwa nyuma katika upatikanaji wa haki na fursa za kimaendeleo'.
Hali kadhalika, Rais Samia amesimama imara kuitetea taswira ya nchi kimataifa kwa kuweka wazi kuwa Tanzania ni mfuasi makini na mzuri sana wa haki za binadamu kupitia mifumo imara ya kisheria na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa.
Amekemea kwa nguvu zote wimbi la sasa linalojaribu kuwaaminisha vijana kuwa serikali za Afrika, hususan ya Tanzania, zinakiuka au hazifuati misingi ya haki za binadamu, akisisitiza kuwa upotoshaji huo hauna nafasi katika taifa linalojali utu na uwajibikaji.
Rais Samia ametoa wito kwa mawakili wote kuhakikisha kuwa taaluma yao haitumiwi kamwe kuhalalisha ajenda zenye nia ovu dhidi ya taifa, bali iendelee kuwa ngao ya kulinda uhuru, amani, na utu wa kila Mtanzania





Social Plugin