
Jeshi la Polisi Tanzania limesema hali ya usalama nchini ni shwari na kwamba litaendelea kupokea taarifa za nia ya kufanya mikutano ya hadhara na vikao mbalimbali kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wengine, huku likiwataka wanaokusudia kufanya mikutano hiyo kuwasilisha taarifa kwa Wakuu wa Polisi wa Wilaya kwa mujibu wa sheria.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatano Julai 29, 2026, Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania, DCP David Misime, amesema uamuzi huo umechukuliwa baada ya hali ya usalama nchini kuendelea kuwa tulivu kufuatia hatua zilizochukuliwa na vyombo vya ulinzi na usalama kudhibiti mipango ya baadhi ya watu waliokuwa wakihamasisha vitendo vya kihalifu.
Amesema katika kipindi hicho Jeshi la Polisi lilikuwa likiwashauri waandaaji wa mikutano kuiahirisha kutokana na mazingira ya kiusalama yaliyokuwapo wakati huo.
DCP Misime amewashukuru Watanzania kwa ushirikiano waliouonesha kwa kuzingatia maelekezo ya vyombo vya ulinzi na usalama na kutoshiriki katika vitendo vya kihalifu vilivyokuwa vinapangwa na kuhamasishwa.
"Walikuwa wakielekezana mbinu watakazotumia kufanikisha malengo yao ikiwa ni pamoja na kuua watu, kuchoma moto shule ili kuleta hofu na taharuki kwa wazazi na walezi na kulipua transfoma za Tanesci, kufunga barabara na kupora askari silaha. Kitendo cha wananchi kuvikataa vitendo hivyo ndicho kilichochangia nchi kuendelea kuwa shwari," alisema.


Social Plugin