Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NAIBU WAZIRI LONDO AWATAKA WAZALISHAJI KUTUMIA HUDUMA ZA TBS


NA EMMANUEL MBATILO, DAR ES SALAAM

UWEKEZAJI unaofanywa katika Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS) umeongeza uwezo wa taasisi hiyo kulinda afya za Watanzania, thamani ya fedha za wananchi na kusaidia bidhaa zinazozalishwa nchini kushindana katika masoko ya ndani na kimataifa.

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dennis Londo, amesema hayo leo Julai 27, 2026 jijini Dar es Salaam wakati wa ziara yake TBS kwa ajili ya kujifunza na kujionea shughuli mbalimbali zinazotekelezwa na taasisi hiyo, ikiwamo kazi za upimaji katika maabara zake.

Londo amesema TBS ni mshirika muhimu wa Serikali katika kuhakikisha bidhaa zinazotumiwa na wananchi zinakidhi viwango vya ubora na usalama, huku wazalishaji wakisaidiwa kuboresha bidhaa zao na kupata fursa ya kufikia masoko mapana zaidi.

Amesema ziara hiyo imempa fursa ya kuzungumza na watumishi wa TBS na kujionea namna taasisi hiyo inavyotekeleza majukumu yake kwa kutumia mashine na vifaa vya kisasa vilivyowezeshwa na Serikali.

“Taasisi hii ni muhimu kulinda afya ya Watanzania, lakini pia kuangalia thamani ya fedha ya Mtanzania kulingana na matumizi ya bidhaa anazotumia inalindwa. Kwa hiyo, kimsingi TBS ni mshirika muhimu ndani ya Wizara ya Viwanda na Biashara,” amesema.

Katika hatua nyingine, Londo amewataka wazalishaji na wajasiriamali kutumia huduma zinazotolewa na TBS bila hofu, akisema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowawezesha kupata huduma za viwango kwa urahisi.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amesema uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali katika maabara za taasisi hiyo umeongeza uwezo wake wa kuhakikisha ubora na usalama wa bidhaa zinazotumiwa na Watanzania.

Katunzi amesema baadhi ya maabara zimewekewa mashine na vifaa vya kisasa vyenye thamani ya mabilioni ya fedha, hali ambayo imeongeza uwezo wa TBS kufanya vipimo mbalimbali kwa ufanisi na kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini na zinazoingizwa zinakidhi viwango vinavyotakiwa.

“Ndani ya maabara zetu tuna uwekezaji mkubwa ambao waandishi wa habari mmeuona katika maabara mbalimbali. Kwa mfano, katika maabara hii ya uchambuzi wa chakula, kuna uwekezaji usiopungua Sh bilioni tano, huku mashine mbalimbali zikifikia takribani Sh bilioni 10 kwenye eneo moja,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com