Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAJASIRIAMALI WATAKA MAENEO MAALUMU YA VIWANDA KILA MKOA



Na Mwandishi Wetu,Dodoma

SERIKALI imeombwa kufikiria kutoa ruzuku kwa Umoja wa Wanawake na Wanaume wa Viwanda Tanzania (WAWAVITA) ili kuimarisha jitihada za kuwainua wanachama wake kiuchumi kupitia sekta ya viwanda.

Mkurugenzi wa WAWAVITA Taifa, Rehema Mbeleke, ameeleza hayo  katika mahojiano Jijini Dodoma 
"Tunaomba serikali itupatie ruzuku. Hii ni taasisi iliyojikita kuendeleza shughuli za wenye viwanda katika mnyororo wa thamani wa uzalishaji. Ruzuku hiyo itatusaidia kuwafikia watu wengi zaidi kwa lengo la kuboresha biashara zao," alisema.

Aidha, aliiomba serikali kuendelea kushirikiana na wenye viwanda vidogo, ikiwemo kutenga maeneo maalumu ya viwanda katika mikoa mbalimbali nchini ili kuwawezesha kuzalisha bidhaa zenye viwango vya ubora na soko la uhakika ndani na nje ya nchi.

Mbeleke alisema wenye viwanda wanatamani kuona serikali ikitenga maeneo hayo maalumu kwa ajili ya shughuli za uzalishaji.

"Uchumi wa viwanda ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa. Tujikite katika uzalishaji wa bidhaa zenye ubora ili tuwe na soko la uhakika ndani na nje ya nchi," alisema.

Alisema hadi kufikia Juni mwaka huu, WAWAVITA ilikuwa na wanachama 26,800 nchini kote, huku Mkoa wa Mwanza na wilaya zake ukiongoza kwa kuwa na wanachama zaidi ya 8,000.

Alieleza kuwa umoja huo ulianzishwa kwa lengo la kuwaunganisha wajasiriamali ili wawe na mikakati ya pamoja ya kujiimarisha kiuchumi na kuibua fursa mbalimbali za maendeleo.

Kwa mujibu wa Mbeleke, bidhaa nyingi za wajasiriamali wadogo huzalishwa majumbani kutokana na ukosefu wa maeneo maalumu ya uzalishaji.

"Changamoto kubwa ya wajasiriamali ni kufanyia kazi majumbani. Katika kukabiliana na hali hiyo, jitihada zimefanyika na wengi wameunganishwa na Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) ili wapate huduma mbalimbali, pamoja na kushirikiana na Taasisi ya Viwango Tanzania (TBS) kupata alama za ubora, hatua inayowezesha bidhaa zao kuingia sokoni kwa urahisi," alisema.

Aliishukuru serikali kupitia SIDO kwa kuendelea kuwawezesha wajasiriamali na kuonyesha dhamira ya kuona Watanzania wanapiga hatua katika maendeleo ya kiuchumi.

Alisema mpango wa baadaye wa WAWAVITA ni kuwa na maeneo ya viwanda katika kila mkoa nchini ili wajasiriamali waweze kufanya shughuli zao katika mazingira rafiki yenye miundombinu stahiki.

"Hapa Dodoma, SIDO tayari ina maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya uzalishaji. Ndoto yetu ni kuona hali hiyo inafikiwa katika kila mkoa ili wajasiriamali waweze kuzalisha, kuingia kwenye masoko na kunufaika na fursa mbalimbali za kiuchumi," alisema.

Aidha, alisema kuwa mkoani Dodoma wameanzisha mfumo wa mobile marketing (masoko yanayotembea), ambao umekuwa ukiwasaidia wajasiriamali kujenga uwezo na kujiamini katika kutangaza na kuuza bidhaa zao.

Aliwahamasisha wenye viwanda na wajasiriamali kujiunga na WAWAVITA ili wanufaike na fursa mbalimbali zinazotolewa na umoja huo.

"Usiidharau fursa. Iwe unatengeneza sabuni ya maji, siagi ya karanga au bidhaa nyingine yoyote, yote ni biashara yenye uwezo wa kukuingizia kipato," alisema.

Aliongeza kuwa WAWAVITA mwaka huu itafanya mkutano wake wa mwaka jijini Dodoma, baada ya mkutano wa mwaka uliopita kufanyika jijini Dar es salaam.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com