
Mashine zinazozalishwa na SIDO Ruvuma chini ya uongozi wa meneja wake Baraka Kandoga.
Na Regina Ndumbaro Songea-Ruvuma
Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma imetenga ekari tano katika Kata ya Ngembambili kwa ajili ya uanzishaji wa Kongano ya Viwanda chini ya usimamizi wa Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), hatua inayolenga kuongeza thamani ya mazao, kukuza viwanda vidogo na vya kati, kuanzisha ajira mpya na kuimarisha uchumi wa wananchi.
Hatua hiyo imeelezwa wakati wa ziara ya kikazi ya Halmashauri ya Mbinga kuja SIDO Mkoa wa Ruvuma kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya shirika hilo na Halmashauri katika kuwawezesha wananchi kupitia maendeleo ya viwanda na biashara.
Akizungumza katika kikao hicho, Meneja wa SIDO Mkoa wa Ruvuma, Baraka Kandoga, amepongeza uamuzi wa Halmashauri ya Mbinga kutenga eneo hilo, akisema kongano ya viwanda itakuwa kitovu cha uzalishaji, ubunifu wa teknolojia na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo hususani mahindi.
Amesema hatua hiyo inaenda sambamba na ushirikiano kati ya SIDO na Ofisi ya Rais – TAMISEMI unaolenga kutumia utaalamu wa SIDO kuwawezesha wanufaika wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri ili mikopo hiyo izalishe biashara endelevu badala ya kuwa chanzo cha kipato cha muda mfupi.
Kandoga amesema SIDO itaendelea kutoa mafunzo ya ujasiriamali, uhamishaji wa teknolojia, usimamizi wa miradi na huduma za maendeleo ya biashara kwa wananchi na vikundi mbalimbali, huku akisisitiza kuwa dira ya Taifa ya maendeleo 2050 inaweka msisitizo mkubwa katika ushirikiano wa Serikali, mamlaka za Serikali za mitaa na wadau wa maendeleo.
Amesema ushirikiano huo utawasaidia wananchi kubadili mawazo yao kuwa miradi ya viwanda, kuongeza ajira kwa vijana na wanawake pamoja na kujenga uchumi jumuishi unaotokana na uzalishaji wa ndani.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Mbinga, Joseph Kashushura, amesema ziara hiyo imewapa fursa ya kujifunza teknolojia na huduma zinazotolewa na SIDO ili ziweze kutumika kuwainua wananchi kiuchumi.
Amesema Halmashauri itaongeza idadi ya wananchi watakaopelekwa kupata mafunzo ya ujasiriamali na teknolojia za uzalishaji, huku ikihamasisha matumizi ya mashine mbalimbali zinazozalishwa na SIDO, ikiwemo za kusaga unga, kutengeneza matofali na vifaa vya kilimo, ili vijana na wanawake wajiajiri na kuongeza kipato chao.
Kashushura amesema Halmashauri imejipanga kuifanya Ngembambili kuwa kitovu cha biashara na uwekezaji kwa kutenga eneo la ekari 173 lenye miundombinu ya barabara, ambapo tayari taasisi mbalimbali zimeanza kuwekeza, huku SIDO ikipewa ekari tano kuanzisha Kongano ya Viwanda.
Amesema lengo ni kuanzisha mkusanyiko wa viwanda vya kuchakata mahindi, kuzalisha unga, vifungashio na bidhaa nyingine zenye thamani ya juu ili kuondokana na uuzaji wa mazao ghafi, kuongeza thamani ya mazao ya wakulima na kuleta mabadiliko ya kweli ya kiuchumi kwa wananchi wa wilaya ya Mbinga na mkoa wa Ruvuma kwa ujumla.



Social Plugin