Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

NDEJEMBI ASHUHUDIA UTIAJI SAINI WA MKATABA WA SH. BILIONI 204.7 KWA MRADI WA UMEME WA JUA KISHAPU

Na Mwandishi wetu - Malunde 1 blog

Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi (Mb), ameshuhudia utiaji saini wa mkataba wenye thamani ya Shilingi bilioni 204.7 kwa ajili ya utekelezaji wa awamu ya pili ya Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu wenye uwezo wa kuzalisha Megawati 100, utakaotekelezwa katika eneo la Ngunga, Wilaya ya Kishapu, Mkoa wa Shinyanga.

Mkataba huo umesainiwa leo, Julai 27, 2026, kati ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na mkandarasi anayetekeleza mradi huo, kampuni za Sagemcom Energy & Telecom SAS na STEG International Services.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Waziri Ndejembi amesema mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kuimarisha mseto wa vyanzo vya uzalishaji wa umeme (energy mix), kwa lengo la kuongeza upatikanaji wa umeme wa uhakika, wa gharama nafuu na unaotokana na vyanzo vya nishati jadidifu.

Ameeleza kuwa mradi huo unatekelezwa kwa awamu mbili zenye uwezo wa kuzalisha jumla ya Megawati 150. Awamu ya kwanza yenye uwezo wa Megawati 50 iligharimu Shilingi bilioni 118.3 na kwa sasa ipo katika hatua za mwisho za utekelezaji.

Kwa mujibu wa Waziri Ndejembi, awamu ya pili yenye uwezo wa Megawati 100, ambayo utekelezaji wake umeanza rasmi kupitia utiaji saini wa mkataba huo, itagharimu Shilingi bilioni 204.7, na kufanya gharama za jumla za mradi kufikia Shilingi bilioni 323.

Amesema mradi huo utachangia kuongeza uzalishaji wa umeme kutoka vyanzo vya nishati jadidifu, kuimarisha uthabiti wa mfumo wa umeme nchini na kusaidia Serikali kufikia malengo ya kuhakikisha Tanzania inakuwa na umeme wa kutosha kukidhi mahitaji ya sasa na ya baadaye.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bw. Lazaro Twange, amesema kusainiwa kwa mkataba wa ujenzi wa Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu Awamu ya Pili wenye uwezo wa kuzalisha megawati 100 ni hatua muhimu katika utekelezaji wa mkakati wa TANESCO wa kuongeza uzalishaji wa umeme kupitia vyanzo vya nishati jadidifu.

"Mhe. Waziri mradi huu wenye thamani ya shilingi bilioni 204.7 utaongeza uimara wa Gridi ya Taifa, kuboresha upatikanaji wa umeme wa uhakika kwa wananchi na sekta za uzalishaji, pamoja na kuchangia utekelezaji wa Dira ya Taifa ya maendeleo nipende kuahidi kuwa TANESCO tutasimamia kwa karibu utekelezaji wa mradi huu ili ukamilike kwa wakati, kwa ubora na kwa kuzingatia viwango vyote vya kitaalamu"ameongeza Bw. Twange.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita, amesema utekelezaji wa Mradi wa Umeme wa Jua wa Kishapu Awamu ya Pili unaonesha imani kubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imeendelea kuwa nayo kwa Mkoa wa Shinyanga kutokana na mazingira mazuri ya uwekezaji na ushirikiano wa wananchi.


Aidha, amebainisha kuwa Serikali ya Mkoa itaendelea kutoa ushirikiano kwa TANESCO, mkandarasi na wadau wote wa mradi ili kuhakikisha utekelezaji wake unakwenda kwa wakati, huku akiwahimiza wananchi kuendelea kulinda miundombinu ya umeme kwani ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya Taifa na ustawi wa vizazi vya sasa na vijavyo.

Hafla ya utiaji saini imehudhuriwa na Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Salome Makamba; Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mboni Mhita; Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Umeme na Nishati Jadidifu, Mhandisi Felchesmi Mramba; Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mhe. Subira Mgalu, pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, Chama cha Mapinduzi na wadau wa sekta ya nishati.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com