Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RC MTAKA AIPONGEZA WMA KUENDELEA KUTOA ELIMU YA VIPIMO KWA WAKULIMA NA WAFANYABIASHARA

Njombe, Julai 30, 2026

Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, ameipongeza Wakala wa Vipimo (WMA) kwa kuendesha kampeni ya kutoa elimu kuhusu matumizi sahihi ya vipimo kwa wakulima na wafanyabiashara wa mazao. 

Amesema kampeni hiyo itaimarisha biashara yenye haki, uwazi na uzingatiaji wa Sheria ya Vipimo, huku ikipunguza migogoro inayotokana na uelewa mdogo wa matumizi ya vipimo.

Akizungumza ofisini kwake baada ya kupokea ujumbe wa WMA, Mtaka amesema elimu hiyo itasaidia kuondoa mkanganyiko unaojitokeza katika biashara ya mazao, hususani kuhusu matumizi ya lumbesa.

Alieleza kuwa baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakikamatwa kwa madai ya kubeba lumbesa kutokana na kutofahamu maana yake halisi. Alifafanua kuwa kujaza mzigo na kuweka kishungi juu yake hakumaanishi kuwa ni lumbesa.

Aidha, amesema mzigo hutambulika kama lumbesa pale unapokuwa na uzito unaozidi kilo 100 hadi kilo 105. Amesema uelewa huu utawasaidia wafanyabiashara na wakulima kuzingatia sheria, kuepuka migogoro na kuongeza uaminifu katika masoko.

Awali, Kaimu Meneja wa WMA Mkoa wa Njombe, Bw. Shabani Ikingu, akiwa na wataalamu kutoka Makao Makuu ya WMA, walimtembelea Mkuu wa Mkoa kwa lengo la kujitambulisha na kueleza dhamira ya kampeni hiyo.

WMA wanaendelea kutembelea wakulima na wafanyabiashara wa mazao, hususani parachichi na viazi, kuwajengea uelewa kuhusu matumizi sahihi ya vipimo na umuhimu wa kuzingatia Sheria ya Vipimo.

Katika kuendeleza kampeni hiyo, WMA imepanga kutoa semina maalumu kwa madiwani na wajasiriamali wa Halmashauri ya Mji wa Njombe tarehe 2 Agosti 2026. Semina hiyo inalenga kuongeza uelewa, kuimarisha ushirikiano kati ya WMA, viongozi na wadau wa biashara, pamoja na kujenga mazingira ya biashara yenye haki na ushindani wa usawa.

WMA inaendelea kusisitiza kuwa elimu ndiyo msingi wa matumizi sahihi ya vipimo na utekelezaji wa Sheria ya Vipimo, hatua itakayochochea ukuaji wa biashara na kulinda maslahi ya wakulima, wafanyabiashara na watumiaji.

#Vipimo Sahihi, Biashara ya Haki; Elimu Kwanza, Maendeleo Endelevu kwa Wote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com