Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

LILIAN LIUNDI: MAZINGIRA WEZESHI NI UFUNGUO WA KUONGEZA USHIRIKI WA WANAWAKE KATIKA SEKTA YA USAFIRI WA UMEME

Mwanzilishi wa Mradi wa Pink Ride na Mkurugenzi Mtendaji wa TGNP aliyemaliza muda wake, Lilian Liundi, akizungumza wakati wa mafunzo kwa wanawake madereva wa bajaji kuhusu usafiri wa umeme na usawa wa kijinsia, yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.
Mwanzilishi Mradi wa Pink Ride wa Wanawake Madereva wa Magari ya Magurudumu Matatu( Bajaj) na Mkurugenzi wa Mtandao wa Jinsia Tanzania TGNP aliyemaliza muda wake, Lilian Liundi amesema mabadiliko kuelekea matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme yanapaswa kuambatana na sera na mazingira wezeshi yatakayoongeza ushiriki wa wanawake katika sekta ya usafiri na kuwawezesha kunufaika na fursa za kiuchumi zinazojitokeza.

Liundi ametoa kauli hiyo alipokuwa akichangia mada akiwa miongoni mwa wajumbe wa jopo la wataalamu wa masuala ya jinsia katika sekta ya usafiri, wakati wa mafunzo ya siku tatu kwa wanawake madereva wa magari ya magurudumu matatu yaliyofanyika katika Ukumbi wa Slipway, jijini Dar es Salaam kuanzia Julai 29 hadi 31, 2026.

Mafunzo hayo yameandaliwa na Shirika lisilo la Kiserikali la OVAH, linalowezesha wanawake vijana kupata mafunzo ya udereva na kumiliki bajaji zinazotumia nishati ya umeme, kwa ufadhili wa GIZ.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Liundi amesema maendeleo ya teknolojia ya usafiri wa umeme yanatoa fursa mpya za ajira, ujasiriamali na uwezeshaji wa wanawake, hivyo ni muhimu kuhakikisha wanawake wanapata maarifa, ujuzi na nafasi ya kushiriki kikamilifu katika sekta hiyo inayokua kwa kasi.

Aidha, amesisitiza kuwa ushiriki wa wanawake katika sekta ya usafiri haupaswi kuonekana kama suala la usawa wa kijinsia pekee, bali ni sehemu ya kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kuharakisha mpito kuelekea matumizi ya nishati safi na rafiki kwa mazingira. Kama ilivyosisitizwa katika sera ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake 2023 pamoja na Dira ya Taifa ya 2050. 

Mafunzo hayo yalilenga kuwajengea washiriki uelewa kuhusu matumizi ya vyombo vya usafiri vinavyotumia nishati ya umeme, fursa zilizopo katika sekta hiyo, pamoja na masuala ya jinsia yanayoweza kuchangia kujenga mazingira salama na jumuishi kwa wanawake.

Washiriki wa mafunzo hayo, ambao wengi wao ni wanawake madereva wa magari ya magurudumu matatu, walipata elimu kuhusu teknolojia ya usafiri wa umeme, namna ya kuitumia kwa ufanisi, pamoja na fursa zinazotokana na mabadiliko ya sekta ya usafiri kuelekea matumizi ya nishati mbadala.

Mafunzo hayo yanatarajiwa kuongeza uelewa wa wanawake kuhusu teknolojia ya usafiri wa umeme, kuwawezesha kutumia fursa zinazojitokeza katika sekta hiyo, na kuchangia kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa kijani.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com