Na mwandishi wetu
Wakati baadhi ya wanaharakati na watumiaji wa mitandao ya Kijamii wakihamasisha maandamano kupitia mitandao ya kijamii kuelekea Julai 7, 2026, vijana wanaoishi katika mazingira magumu ambao walijikuta katikati ya vurugu zilizotokea Oktoba 29, 2025 wameeleza namna walivyobeba mzigo mkubwa wa madhara, wakisema hawatamani kuona hali kama hiyo ikijirudia.
Vijana hao wanasema kipindi hicho kilisababisha kukosekana kwa amani, chakula, sehemu za kulala na shughuli za kujipatia kipato, huku baadhi ya wenzao wakijeruhiwa, kupata ulemavu wa kudumu na wengine kupoteza maisha.
Mmoja wao, Juma Maftah, mkazi wa Ilala Dar Es Salaam amesema siku za vurugu zilikuwa ngumu zaidi kwa watu wanaoishi mitaani kuliko kundi lolote lingine.
“Tarehe 29, 2025 wakati ule kilichotokea ilikuwa changamoto sana kwangu, amani hakuna, kula ilikuwa tabu, sehemu za kulala pia kwa sisi tunaolala nje ilikuwa changamoto sana, wengine walivunjika miguu na ndugu zetu wengine walikufa.
Ilifika hatua mpaka tukawa tunakamata mbwa mtaani na kuwala kwa siku siku ambazo zilikuwa na ukosefu wa amani kwa sisi tunaoishi katika mazingira magumu. Mimi niombe vijana wenzangu tusikubali hata kidogo kushawishika tukaingia kwenye kufanya vurugu kwani tutaishia jela, kujisababishia ulemavu au kifo. Amani ndio kila kitu kwenye maisha,” alisema.
Kwa upande wake, Baraka Richard amesema wakati wa vurugu hizo hakuweza kufanya shughuli zake za kubeba mizigo sokoni, akiwataka Vijana wengine Nchini kutokubali kushawishiwa na wito wa kushiriki maandamano au vurugu zinazoweza kuhatarisha maisha yao, wakisema uzoefu wao unaonesha kuwa matokeo yake huacha majeraha ya muda mrefu kwa watu wa kawaida.
Ripoti ya Tume ya Uchunguzi iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Mohamed Othman Chande kuhusu matukio ya vurugu yaliyotokea baada ya uchaguzi wa mwaka 2025 ilibainisha kuwa baadhi ya vijana wanaoishi katika mazingira magumu, maeneo ya stendi na masokoni walirubuniwa kushiriki maandamano kwa kuahidiwa fedha pamoja na ajira.
Ripoti hiyo ilionya kuhusu matumizi ya vijana walio katika mazingira magumu kwa maslahi ya kisiasa, ikisisitiza umuhimu wa kuongeza uelewa na fursa za kiuchumi ili kuwakinga dhidi ya ushawishi unaoweza kuwaingiza kwenye migogoro na vitendo vya vurugu.

Social Plugin