
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Richard Abwao, amefariki dunia leo Jumamosi, Juni 20, 2026, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) jijini Dar es Salaam, ambako alikuwa akiendelea na matibabu.
Kifo hicho kimethibitishwa na Jeshi la Polisi kupitia Msemaji wake, DCP David Misime, ambaye amesema SACP Abwao amefariki dunia leo baada ya kuugua na kuwa chini ya uangalizi wa madaktari katika hospitali hiyo.
"Ni kweli aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi Richard Abwao, amefariki dunia leo tarehe 20 Juni 2026 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili alikokuwa akipatiwa matibabu," amesema DCP Misime.
Ameongeza kuwa taarifa zaidi kuhusu chanzo cha ugonjwa wake pamoja na ratiba za mazishi zitatolewa na familia pamoja na mamlaka husika.
Akizungumzia msiba huo, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha, amesema kifo cha SACP Richard Abwao ni pigo kubwa kwa Jeshi la Polisi na wananchi wa Mkoa wa Tabora kutokana na mchango wake mkubwa katika kuimarisha usalama, amani na utulivu wa mkoa huo.
"Kwa masikitiko makubwa nimepokea taarifa ya kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, SACP Richard Abwao, kilichotokea leo. Hii ni taarifa iliyotushtua sana sisi viongozi wa Mkoa wa Tabora, vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na wananchi wote wa Mkoa wetu.
Katika kipindi chake cha utumishi mkoani Tabora, Marehemu SACP Richard Abwao alikuwa kiongozi mwenye ushirikiano mkubwa, aliyesimamia kwa weledi, uzalendo na kujitoa kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unalindwa wakati wote. Alikuwa karibu na wananchi, akisikiliza changamoto zao na kushirikiana na Kamati ya Ulinzi katika kudumisha amani na utulivu wa Mkoa wetu.
Kwa niaba yangu binafsi na kwa niaba ya Serikali ya Mkoa wa Tabora, ninatoa pole zangu za dhati kwa Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP) Camillius Wambura, familia ya marehemu, Kamati ya Ulinzi ya Mkoa, askari wote wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Tabora pamoja na wananchi wote wa Mkoa wa Tabora kwa msiba huu mzito.
Tumeondokewa na kiongozi, mtumishi na mshiriki mkubwa wa juhudi za kulinda amani yetu.
Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. Amina", amesema
Kifo cha SACP Richard Abwao kimeacha simanzi kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki, viongozi wa serikali, askari wa Jeshi la Polisi pamoja na wananchi wengi waliopata fursa ya kufanya kazi naye katika kipindi cha utumishi wake.
Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi. Amina.
Social Plugin