
Azam FC imeweka historia nyingine muhimu katika msimu huu baada ya kuiondoa Yanga SC kwenye mbio za ubingwa wa Kombe la Shirikisho la CRDB Bank Federation Cup kwa ushindi wa mabao 3-2 katika mchezo mkali wa nusu fainali uliochezwa leo, Juni 21, 2026, kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza.
Mchezo huo ulilazimika kuchezwa hadi dakika 120 ili kumpata mshindi baada ya timu hizo kutoka sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 za muda wa kawaida.
Azam FC walikuwa wa kwanza kupata bao dakika ya 28 kupitia kwa Himid Mao Mkami na kwenda mapumziko wakiwa mbele kwa bao 1-0.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi huku Yanga SC wakifanikiwa kusawazisha dakika ya 67 kupitia kwa Prince Dube. Hata hivyo, Azam FC walirejesha uongozi dakika ya 85 baada ya Lameck Lawi kuifungia timu hiyo bao la pili.
Yanga SC waliendelea kupambana na kufanikiwa kusawazisha tena kupitia kwa Bakari Mwamnyeto, hatua iliyoufanya mchezo kumalizika kwa sare ya mabao 2-2 ndani ya muda wa kawaida.
Katika muda wa nyongeza, Jephté Kitambala alijitokeza kuwa shujaa wa Azam FC baada ya kufunga bao la tatu na la ushindi dakika ya 112, lililoihakikishia timu hiyo tiketi ya kutinga fainali ya michuano hiyo.
Kutokana na ushindi huo, Azam FC imefuzu kucheza fainali ya CRDB Bank Federation Cup ambapo itakutana na Simba SC katika pambano la kuwania ubingwa wa mashindano hayo.
Social Plugin