Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TRA YAELEZA SIRI YA MAFANIKIO ULIPAJI KODI KWA HIARI

Meneja wa TRA mkoa Kigoma Beatus Nchota
Zuwena Hussein Mwenyekiti wa SHIUMA Halmashauri ya wilaya Kigoma

Na Fadhili Abdallah,Kigoma

Mamlaka ya mapato (TRA) mkoa Kigoma imesema kuwa ongezeko kubwa la wafanyabiashara wa mkoa huo kulipa kodi kwa hiari kunachangiwa na mikakati mbalimbali iliyowekwa na mamlaka hiyo ikiwemo utoaji elimu ya kodi, kuboresha mazingira ya biashara, pamoja na kujenga mahusiano mazuri kati ya TRA na wafanyabiashara.
 
Meneja wa TRA mkoa Kigoma, Beatus Nchota alisema hayo akikabidhi samani za ofisi zilizotolewa na mamlaka hiyo ofisi ya mkoa Kigoma kwa viongozi wa Shirikisho la Umoja wa Machinga (SHIUMA) katika halmashauri ya  wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma.
 
Nchota alisema kuwa utoaji wa elimu ya kodi umekuwa nguzo muhimu katika kuwajengea wafanyabiashara uelewa wa wajibu wao wa kulipa kodi na faida za kufanya hivyo kwa hiari. Kupitia semina, mikutano ya wadau, ziara za elimu katika maeneo ya biashara na matumizi ya vyombo vya habari, wafanyabiashara wamepata fursa ya kuelewa sheria za kodi, taratibu za ulipaji pamoja na umuhimu wa kodi katika maendeleo ya taifa.
 
Sambamba na hilo, Nchota alisemaa kuwa TRA Mkoa wa Kigoma imefanikiwa kujenga uhusiano wa karibu na wafanyabiashara kwa kuzingatia huduma bora kwa walipa kodi ambapo mamlaka hiyo imekuwa ikisikiliza changamoto za wafanyabiashara, kutoa ushauri wa kitaalamu na kutatua kero zinazoweza kuathiri utekelezaji wa majukumu ya kodi, hatua hiyo imeongeza imani na ushirikiano kati ya TRA na wfanyabiashara wa mkoa huo.
 
 Katika hatua nyingine meneja huyo alisema kuwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Kigoma imekuja na mpango mkakati maalumu unaolenga kuinua wafanyabiashara wadogo ili kukuza biashara zao na hatimaye kuingia kwenye mfumo rasmi wa ulipaji kodi.

Akizungumza na wafaanyabiashara hao Nchota alisema kuwa mamlaka hiyo imebaini kuwa wafanyabiashara wengi wadogo wana uwezo wa kukuza biashara zao lakini wanakabiliwa na changamoto za uelewa wa masuala ya usimamizi wa biashara, utunzaji wa kumbukumbu za mapato na matumizi pamoja na fursa za masoko.


“Lengo letu si kukusanya kodi pekee, bali pia kuona wafanyabiashara wanakua kiuchumi. Tunapotumia elimu ya biashara kuwajengea uwezo, tunawawezesha kuongeza mauzo, kupata faida zaidi na hatimaye kuingia kwenye wigo wa ulipaji kodi kwa hiari,” alisema Nchota.

Akizungumzia msaada wa samani uliotolewa kwa Shirikisho hilo la Umoja wa Machinga Meneja huyo wa TRA alisema kuwa unalenga kuwatia moyo na kuwaunga mkono ili biashara zao zikue na kuweza kulipa kodi Zaidi kwa biashara wanazofanya kwani hata sasa wanaponunua bidhaa hizo na kuja kuuza pia zimekuwa zikikatwa
 
Wakizungumza baada ya kupokea samani hizo viongozi wa SHIUMA Halmashauri ya wilaya Kigoma akiwemo Mwenyekiti wa Umoja huo, Zuwena alisema kuwa kwa sasa TRA imekuwa ikifanya kazi kama mshirika kwa kusikiliza changamoto za biashara  wanapokuja kwenye biashara zao badala ya kuwa taasisi ya usimamizi pekee si kama ilivyokuwa hapo awali jambo linalochangia wafanyabiashara kulipa kodi kwa hiari na kuwepo kwa ongezeko la walipa kodi wapya.
 
zuwena alisema kuwa anaamini mahusiano hayo yataimarika zaidi na kwamba kutolewa kwa samani hizo kunarudisha imani ya wafanyabiashara kwa TRA kukiona kama chombo chao hivyo kuwa na moyo wa kuinia kama walipa kodi wapya lakini pia kulipa kodi kwa hiari.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com