Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TEA YATAKIWA KUONGEZA ELIMU KWA UMMA KUHUSU FURSA ZA MFUKO WA ELIMU WA TAIFA

Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, akisikiliza maelezo kutoka kwa timu ya wataalamu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), alipotembelea banda la maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea viwanja vya Chinangali Dodoma

**********

Dodoma – Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imetakiwa kuongeza juhudi katika kutoa elimu kwa umma na wadau mbalimbali kuhusu namna Mfuko wa Elimu wa Taifa unavyofanya kazi pamoja na fursa zinazopatikana kupitia mfuko huo, ili kuongeza mchango wake katika maendeleo ya sekta ya elimu nchini.

Wito huo umetolewa leo na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, wakati alipotembelea banda la maonesho la TEA katika Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea jijini Dodoma.

Akizungumza baada ya kupokea maelezo kutoka kwa wataalamu wa TEA, Bw. Mkomi amesema mamlaka hiyo imekuwa ikifanya kazi kubwa na ya mfano katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini. Hata hivyo, amesisitiza umuhimu wa wananchi na wadau wengi zaidi kufahamu taratibu za kuchangia na kunufaika na Mfuko wa Elimu wa Taifa.

“TEA ina mchango mkubwa katika kuimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia. Ni muhimu sasa kuongeza uhamasishaji ili wananchi wengi zaidi wafahamu fursa zilizopo na namna wanavyoweza kushiriki katika kuendeleza sekta ya elimu kupitia mfuko huu,” amesema Bw. Mkomi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa TEA, Bi. Bestina Magutu, amemshukuru Katibu Mkuu huyo kwa maelekezo yake na kueleza kuwa mamlaka hiyo itayafanyia kazi kwa ufanisi mkubwa.

Bi. Magutu amesema TEA imejipanga kutumia majukwaa mbalimbali ya mawasiliano, ikiwemo vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, ili kuhakikisha elimu kuhusu Mfuko wa Elimu wa Taifa inawafikia wananchi katika maeneo mbalimbali hapa nchini.

Mfuko wa Elimu wa Taifa unasimamiwa na Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) ukiwa na jukumu la kutafuta rasilimali fedha na vifaa kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya elimu nchini, hususan katika maeneo yenye mahitaji makubwa.

Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma ya mwaka 2026 yanafanyika chini ya kaulimbiu isemayo: “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu.”
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, akipokea zawadi kutoka kwa Bi. Eliafile Solla, Afisa Uhusiano na Mawasiliano wa TEA alipotembelea banda la maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea viwanja vya Chinangali Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, akisisitiza jambo alipotembelea banda la maonesho la TEA kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea viwanja vya Chinangali Dodoma
Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, akisikiliza maelezo kutoka kwa timu ya wataalamu Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), alipotembelea banda la maonesho kwenye maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea viwanja vya Chinangali Dodoma

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com