Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAKUKURU TANGA YAOKOA ZAIDI YA SHILINGI MILIONI 116 KUPITIA MFUMO WA NeST


Na Hadija Bagasha, Tanga

Mfumo wa Kielektroniki wa Ununuzi wa Umma (NeST) umeendelea kuonyesha umuhimu wake katika kuimarisha uwazi na ufanisi wa matumizi ya fedha za umma baada ya kufichua mapungufu makubwa yaliyokuwa yakikwamisha utekelezaji wa miradi ya elimu mkoani Tanga, hatua iliyosaidia kuokoa zaidi ya Shilingi milioni 116.2 zilizokuwa katika hatari ya kupotea.

Hayo yameelezwa leo Juni 8, 2026 na Kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Tanga, Ramadhan Ndwata, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli za taasisi hiyo katika robo ya kwanza ya mwaka kuanzia Januari hadi Machi 2026.

Kamanda Ndwata alisema kuwa ufuatiliaji wa karibu uliofanywa na TAKUKURU katika miradi mbalimbali ya maendeleo umebaini dosari kadhaa zilizokuwa zikisababisha ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi ya elimu licha ya Serikali kuwa tayari imetoa fedha kwa ajili ya utekelezaji wake.

Alieleza kuwa moja ya miradi iliyobainika kuwa na changamoto ni ule wa ujenzi wa madarasa mawili pamoja na vyoo katika Shule ya Sekondari Chongoleani. Kwa mujibu wa Ndwata, mradi huo ulikwama kwa muda mrefu tangu Machi 2024 kutokana na makadirio ya gharama za manunuzi kuwa chini ya bei halisi ya soko, jambo lililosababisha mfumo wa NeST kukataa zabuni zote zilizowasilishwa kwa kuwa hazikukidhi vigezo vya kitaalamu.

Aidha, alisema kuwa katika mradi wa ujenzi wa vyoo wenye thamani ya Shilingi milioni 40 katika shule hiyo, hakukuwa na makadirio ya gharama yaliyoandaliwa, hali iliyosababisha mchakato mzima wa manunuzi kushindwa kuanza na hivyo kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo muhimu kwa wanafunzi.

“Kwa upande wa ujenzi wa vyoo vya Shilingi milioni 40 katika Shule ya Sekondari Chongoleani, hakukuwa kabisa na makadirio ya gharama yaliyoandaliwa jambo lililosababisha mchakato kushindwa kuanza. Tulichukua hatua za dharura na kwa sasa mradi umerudi katika utekelezaji na unaendelea vizuri,” alisema Ndwata.

Katika hatua nyingine, TAKUKURU Mkoa wa Tanga imefanikiwa kuingilia kati na kufuatilia kwa karibu mradi mkubwa wa ujenzi wa Shule ya Sekondari Kwabastola wilayani Muheza wenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni moja.
Kupitia ufuatiliaji huo, taasisi hiyo ilibaini uwepo wa kazi zilizokuwa zimefanyika chini ya kiwango na kuagiza marekebisho ya haraka ili kuhakikisha thamani ya fedha za Serikali inalindwa.

 Baadhi ya kazi zilizolazimika kukamilishwa ni pamoja na upakaji wa vanish kwenye milango, marekebisho ya kazi za gypsum pamoja na kuhakikisha vifaa muhimu vya shule vinapatikana kwa wakati.

Ndwata alisema kuwa TAKUKURU pia ilisimamia ununuzi wa vitanda 57 vyenye thamani ya Shilingi milioni 22.4 kwa ajili ya shule hiyo, huku vitanda vingine 23 vilivyokuwa vimehamishiwa katika shule jirani vikielekezwa kurejeshwa ili kutumika kwa madhumuni yaliyokusudiwa.

Mbali na shughuli za ufuatiliaji wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU Mkoa wa Tanga imeendelea kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa kupitia elimu kwa umma. 

Katika kipindi hicho, wananchi 189,521 walifikiwa kupitia semina, mikutano ya hadhara, vipindi vya uelimishaji pamoja na klabu za wapinga rushwa katika shule mbalimbali.

Kamanda Ndwata alisema elimu hiyo imelenga kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu athari za rushwa na umuhimu wa kushiriki kikamilifu katika kulinda rasilimali za umma kwa manufaa ya jamii nzima.

Kwa upande wa utekelezaji wa sheria, TAKUKURU Mkoa wa Tanga ilipokea jumla ya malalamiko 133 katika robo ya kwanza ya mwaka, ambapo malalamiko 100 yalihusiana moja kwa moja na tuhuma za vitendo vya rushwa.

Alisema uchunguzi wa malalamiko hayo umeendelea kufanyika kwa mujibu wa sheria, huku baadhi ya kesi zikifikishwa mahakamani. 

Hadi sasa, jumla ya kesi 11 mpya zimefunguliwa mahakamani na kesi nyingine 18 zinaendelea kusikilizwa katika mahakama mbalimbali mkoani Tanga.

Akizungumzia mipango ya kipindi cha Aprili hadi Juni 2026, Ndwata alisema TAKUKURU itaendelea kuimarisha uchambuzi wa mifumo ya utendaji kazi katika taasisi za umma kwa lengo la kubaini na kuziba mianya inayoweza kusababisha rushwa na ubadhirifu wa mali za umma.

Aidha, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa na ubadhirifu ili kuhakikisha rasilimali za taifa zinalindwa na kutumika kwa manufaa ya wananchi wote.

“Mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushirikiano wa kila mwananchi.

 Tunapaswa kulinda rasilimali za taifa ili ziweze kuleta maendeleo na kuboresha maisha ya Watanzania wote,” alisisitiza Ndwata.

Hatua hizo zinaonyesha namna matumizi ya mifumo ya kidijitali kama NeST pamoja na ufuatiliaji wa karibu wa taasisi za uwajibikaji yanavyoweza kusaidia kuongeza uwazi, kuimarisha usimamizi wa fedha za umma na kuhakikisha miradi ya maendeleo inatekelezwa kwa wakati na kwa viwango vinavyostahili.






Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com