Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

TAFITI ZA NDANI ZATAKIWA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA YA AKILI


Na Farida Mangube, Morogoro

Wataalamu wa saikolojia nchini wameeleza kuwa ukosefu wa tafiti zinazoakisi uhalisia wa jamii za Kitanzania, pamoja na kuendelea kutegemea nadharia za Magharibi, bado ni kikwazo kikubwa katika juhudi za kukabiliana na changamoto za afya ya akili zinazoongezeka nchini.

Kauli hiyo imetolewa katika Kongamano la Tatu la Kisayansi na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania (TAPA) unaoendelea mkoani Morogoro, ambapo washiriki wamesisitiza umuhimu wa kuwekeza katika tafiti zinazozingatia mazingira, tamaduni na mahitaji halisi ya jamii za Kitanzania ili kuboresha elimu ya saikolojia na huduma za afya ya akili.

Akizungumza nje ya mkutano huo uliuokwenda sambamba na uchaguzi  Rais mpya wa TAPA Barnabas  Nkinga amesema chama kitaendelea kuhamasisha tafiti za kisayansi zinazolenga mazingira ya Tanzania, kuimarisha ushirikiano kati ya wataalamu na taasisi mbalimbali, pamoja na kuhakikisha maazimio ya kongamano hilo yanatekelezwa kwa vitendo.

Amesema tafiiti zitasaidia kuifanya taaluma ya saikolojia kutoa suluhisho yanayokidhi changamoto zinazowakabili wananchi na kuchangia katika kuboresha huduma za afya ya akili nchini.

Baadhi ya washiriki wa kongamano hilo  akiwemo Charles Deogratius wameitaka Serikali na wadau wa sekta ya afya kuongeza uwekezaji katika tafiti za ndani, wakisema utegemezi wa nadharia za Magharibi pekee umekuwa ukikwamisha upatikanaji wa mbinu zinazolingana na mazingira ya Kitanzania.

Pia wameutaka uongozi mpya wa TAPA kusimamia kwa karibu utekelezaji wa maazimio yatakayopitishwa ili taaluma ya saikolojia iweze kutoa mchango mkubwa zaidi katika kukabiliana na changamoto za afya ya akili nchini.

Kongamano la Tatu la Kisayansi pamoja na Mkutano Mkuu wa 10 wa Chama cha Wanasaikolojia Tanzania limehitimishwa kwa kupitisha maazimio yatakayokuwa mwongozo wa kuimarisha tafiti, elimu ya saikolojia na huduma za afya ya akili nchini. Uongozi mpya wa chama unatarajiwa kuanza rasmi kuyasimamia na kuyatekeleza maazimio hayo.




Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com