Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

SERIKALI YAPONGEZA UJIO WA VYUO VIKUU BORA VYA MALAYSIA TANZANIA


Na Mwandishi Wetu

WAZAZI na wanafunzi nchini wamefurahishwa na maonesho ya vyuo vikuu Malaysia ambavyo vimewapa fursa mbalimbali za masomo nchini humo kwenye maonesho yaliyofanyika jana.

Akizungumza kwenye maonesho hayo, Mratibu wa maonesho, ambaye ni Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Elimu Vyuo Vikuu, Global Education Link, (GEL), Abdulmalik Mollel, alisema maonesho yametoa fursa nyingi kwa vijana.

Alisema vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini wamefika kwenye maonesho hayo na kwamba kama kuna waliokosa nafasi wafike Global Education Link ambako watapatiwa fursa kama hiyo ya kuvijua vyuo hivyo

“GEL inawahimiza wanafunzi, wazazi na walezi waliokosa kuhudhuria Maonesho ya Study in Malaysia katika Hoteli ya Serena kufika ofisi za GEL, ambako huduma za ushauri, udahili, scholarship na mwongozo wa kusoma Malaysia zinaendelea kutolewa kama ilivyokuwa kwenye maonesho,” alisema Mollel.

Mollel alisema maonesho hayo ya Study in Malaysia yamefungua fursa za Scholarship kwa wanafunzi wa Tanzania na kuongeza kuwa wazazi, walezi na wanafunzi waliohudhuria maonesho hayo Serena Hotel wameeleza kufurahishwa na fursa za scholarship, udahili wa moja kwa moja na mwongozo wa kusoma Malaysia.

Mollel alisema vyuo vikuu vya Tanzania na Malaysia vitajenga ushirikiano mpya wa elimu ya juu na kwamba maonesho hayo yamefungua milango ya ushirikiano katika tafiti, programu za 2+2, ubadilishanaji wa wanafunzi na wahadhiri pamoja na uhusiano wa kitaaluma.

Alisema Serikali imeeleza kuwa ujio huo unaunga mkono jitihada za kuimarisha elimu ya juu, kuongeza ushirikiano wa kimataifa na kuwajengea vijana uwezo wa kushindana duniani.

Alisema washiriki wa maonesho wamepata nafasi ya kukutana moja kwa moja na wawakilishi wa vyuo, kuuliza maswali kuhusu ada, scholarship, visa, kozi na maisha ya mwanafunzi Malaysia.

Aidha, alisema maonesho ya Study in Malaysia yamewakutanisha wanafunzi wa Tanzania na vyuo vikuu vinavyotambulika kimataifa kwa taaluma za afya, teknolojia, biashara, uhandisi na ubunifu.

Alisema Global Education Link kwa kushirikiana na Education Malaysia Global Services wamefanikisha maonesho yaliyolenga udahili, scholarship na kuimarisha mahusiano ya elimu kati ya Tanzania na Malaysia.

“Vyuo vya Tanzania na Malaysia vimejadili namna ya kuanzisha programu za pamoja zitakazowezesha wanafunzi kusoma sehemu ya masomo Tanzania na kuendelea Malaysia,” alisema Mollel .

Alisema kupitia maonesho hayo, wanafunzi wamepata taarifa za kozi, vigezo vya udahili, fursa za ufadhili na namna ya kujiandaa kwa elimu ya kimataifa.

Alisema vyuo vya Malaysia na Tanzania vitashirikiana kwaajili ya kujenga daraja la muda mrefu kati ya vyuo vya Tanzania na Malaysia katika sayansi, teknolojia, utafiti na maendeleo ya rasilimali watu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com