SERIKALI imezitaka taasisi binafsi za elimu kuendelea kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa mageuzi ya elimu yanayolenga kuimarisha ujuzi, sayansi na teknolojia, huku ikiipongeza Shule ya Kimataifa ya Luminous kwa mchango wake katika kukuza ubora wa elimu nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Mtendaji Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Elimu (ADEM), Dkt. Maulid J. Maulid, alipomwakilisha Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Wanu Hafidh Ameir, katika Mahafali ya Pili ya Shule ya Kimataifa ya Luminous yaliyofanyika Juni 14, 2026 jijini Dar es Salaam.
Dkt. Maulid alisema Serikali imeendelea kufanya maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo pamoja na mitaala ili kuhakikisha mfumo wa elimu unazalisha wahitimu wenye ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na maendeleo ya teknolojia.
Aidha, alibainisha kuwa Serikali inajiandaa kukabiliana na ongezeko kubwa la wanafunzi watakaojiunga na elimu ya sekondari ifikapo mwaka 2028, hali inayotarajiwa kuongeza mahitaji ya miundombinu na rasilimali nyingine za elimu.
“Ushirikiano wa sekta binafsi ni muhimu katika kuhakikisha tunapata miundombinu na mazingira bora ya kujifunzia yatakayokidhi ongezeko la wanafunzi linalotarajiwa katika miaka ijayo,” alisema.
Sambamba na hilo, Dkt. Maulid aliwapongeza wazazi na walezi kwa kuendelea kuwekeza katika elimu na malezi ya watoto wao, akieleza kuwa mchango wao ni msingi muhimu katika kujenga kizazi chenye maarifa, maadili na uzalendo.
Pia alisisitiza kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki yatakayowezesha taasisi za elimu za umma na binafsi kutoa huduma bora zaidi kwa manufaa ya taifa.
Kwa upande wake, uongozi wa Shule ya Kimataifa ya Luminous uliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha mazingira yanayowezesha sekta binafsi kushiriki kikamilifu katika utoaji wa elimu.
Uongozi huo ulisema upo tayari kuendelea kushirikiana na Serikali katika juhudi za kuboresha sekta ya elimu, huku ukitambua mchango wa mifumo na sera mbalimbali zilizowekwa katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora na yenye ushindani wa kimataifa.



















Social Plugin