
Huduma Mbalimbali za kisheria zinazotolewa na Wizara ya Katiba na Sheria zimekuwa chachu na zenye mchango mkubwa katika kuwawezesha wananchi kupata haki, ushauri wa kisheria na utatuzi wa changamoto mbalimbali za kisheria kwa urahisi na kwa wakati.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, akimwakilisha Katibu Mkuu Kiongozi, Dkt. Moses Kasiluka, wakati alipotembelea banda la wizara hiyo wakati wa Maadhimisho ya Kitaifa ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026 kwa kutembelea mabanda mbalimbali ya taasisi za umma yaliyoshiriki maonesho hayo Juni 23, 2026 Viwanja vya Chinangali Jijini Dodoma.
Mara Baada ya kupokea maelezo kutoka kwa wataalamu wa Wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Shemdoe aliipongeza Wizara hiyo kwa jitihada kubwa inazoendelea kuzifanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma za kisheria kwa urahisi, jambo ambalo limechangia kuimarisha uelewa wa wananchi kuhusu haki zao na taratibu mbalimbali za kisheria.
Amesema huduma zinazotolewa na Wizara hiyo zimekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaokumbana na changamoto mbalimbali za kisheria, huku akibainisha kuwa uwepo wa wataalamu katika maonesho hayo umetoa fursa kwa wananchi kupata ushauri na mwongozo wa haraka kuhusu masuala yanayowakabili.
Prof. Shemdoe ameshauri Wizara ya Katiba na Sheria kuendelea kuimarisha ushirikiano na taasisi nyingine za umma pamoja na wadau mbalimbali waliopo karibu na wananchi ili kurahisisha utoaji wa huduma za kisheria na kupunguza changamoto zinazowafikisha wananchi katika ngazi za juu za Serikali.
Ameeleza kuwa changamoto nyingi zinazowasilishwa Wizara ya Katiba na Sheria mara nyingi huanzia katika taasisi au ofisi nyingine za umma, hivyo kuna umuhimu wa kujenga mifumo madhubuti ya ushirikiano, uratibu na utatuzi wa changamoto hizo katika ngazi za awali kabla hazijafikia Wizara husika.
Aidha, amesisitiza kuwa ushirikiano huo utasaidia kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kuokoa muda na gharama kwa wananchi pamoja na kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi za Serikali zinazohusika na utoaji wa huduma mbalimbali.
Wizara ya Katiba na Sheria itaendelea kutekeleza maelekezo hayo kwa kuimarisha ushirikiano na taasisi mbalimbali, kuendeleza utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi na kuhakikisha huduma za msaada wa kisheria zinafika kwa wananchi wengi zaidi kwa lengo la kuimarisha upatikanaji wa haki nchini huku ikidumisha kauli mbiu ya maonyesho hayo isemayo “Kuchochea Uwajibikaji Jumuishi kwa Huduma Endelevu”


Social Plugin