Na mwandishi wetu, Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na uwekezaji Prof. Kitila Alexander Mkumbo amesisitiza kwamba Tanzania inatawaliwa na kuongozwa na misingi ya kidemokrasia na utawala wa sheria na utawala bora, akibainisha kwamba serikali ya Chama Cha Mapinduzi CCM inaenda kutekeleza ahadi yake ya kupatikana kwa Katiba mpya kama ilivyoahidi katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzannia wa Mwaka 2025.
Waziri Kitila Mkumbo amebainisha hayo leo Jumanne Juni 23, 2026, Bungeni Mjini Dodoma wakati akihitimisha mjadala wa taarifa ya uchumi na mpango wa Taifa wa maendeleo, akiwakosoa wale wanaoitisha maandamano na kueleza kuwa hakuna Chama kingine chenye ajenda ya kupatikana kwa Katiba mpya nje ya Chama tawala kinachounda serikali.
'Rais Samia ameweka wazi pia dhamira yake katika kuimarisha utawala wa sheria, uadilifu, haki na uwajibikaji na mapambano dhidi ya rushwa na alipofungua Bunge aliweka msingi wa mambo hayo akisema ili kuhakikisha wananchi wananufaika na rasilimali za Nchi na kupata huduma wanazostahili, ataelekeza jitihada kwenye mapambano dhidi ya rushwa, ufisadi, ubadhirifu, uzembe, ukosefu wa nidhamu na maadili, akisema ni lazima kudhibiti wachache wanaotaka kuturudisha nyuma kwa kuingiza maslahi binafsi." Amesema Waziri Kitila.
Katika maelezo yake, waziri huyo amezisifu pia sera za msingi wa CCM, akisema kinachowaunganisha wanachama wa Chama hicho ni fikra na itikadi na imani kuwa binadamu wote ni sawa na kila mmoja anapaswa kuheshimiwa kwa utu wake, Ilani ikisisitiza pia imani yake katika misingi ya utawala bora, demokrasia, haki za binadamu na utawala wa sheria ni muhimu katika kuhakikisha Taifa linaendelea kuwa na amani na utulivu.

Social Plugin