Katibu Tawala wilayani Kishapu mkoani Shinyanga Fatma Mohamed akizungumza kwenye kikao cha kujadili taarifa za utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji kwa kipindi hicho kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya wilaya ya kishapu Juni 11, 2026
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga imefanikiwa kufikia asilimia 100 ya utoaji wa huduma za chakula na lishe mashuleni kwa angalau mlo mmoja katika kipindi cha robo ya Januari hadi Machi 2026.
Mafanikio hayo yamebainishwa Juni 11, 2026, cha kujadili taarifa za utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji kwa kipindi hicho kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa kikao cha tathmini ya utekelezaji mkataba wa lishe ngazi ya kata , ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Katibu Tawala wa Wilaya, Fatma Mohamed, amewaagiza maafisa wote wanaosimamia afua za lishe kuanzia ngazi ya Wilaya hadi Vijiji kuendelea kutoa elimu kuhusu umuhimu wa lishe bora, hususan kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari.
"Niendelee kuwakumbusha kuwa ustawi wa ufaulu kwa watoto wetu unategemea pia uzingatiaji wa lishe bora mashuleni. Mikakati na mipango yote tuliyonayo kama wilaya kuhusu kuongeza ufaulu haitafanikiwa kama tutaendelea kulichukulia suala hili kuwa la kawaida. Ndiyo maana limepewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan. Hivyo basi, tusiridhike na asilimia hizi 100 bali tuendelee kusimamia na kutekeleza majukumu yetu kikamilifu," amesema Fatma.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwapatia wajawazito elimu kuhusu lishe bora pamoja na matumizi sahihi ya vidonge vya FEFO ili kuhakikisha wanakua na wingi wa damu wa kutosha
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amewapongeza watendaji wa Kata na wadau mbalimbali waliochangia kwa kiasi kikubwa kufanikisha utekelezaji wa afua za lishe na kufikia kiwango hicho cha mafanikio.
Amesema ataendelea kutoa kipaumbele katika kutenga fedha za lishe kwa wakati ili kuhakikisha shughuli zote zinazohusiana na lishe zinatekelezwa kwa ufanisi kulingana na maelekezo yaliyowekwa.
"Mafanikio haya makubwa tunayoyashuhudia leo yametokana na ushirikiano mzuri pamoja na uongozi thabiti wa Mkuu wetu wa Wilaya ambaye amekuwa mstari wa mbele kushiriki maadhimisho ya siku ya afya na lishe vijijini pamoja na kuhamasisha usimamizi na ufuatiliaji wa afua hizi," amesema Johnson.
Pia amewashukuru wadau wa maendeleo wanaotekeleza miradi mbalimbali ndani ya Wilaya hiyo kwa kuendelea kuchangia utekelezaji wa afua za lishe katika shule zilizopo maeneo yao ya miradi. Aidha, ameendelea kuwapongeza wananchi kwa mwitikio mkubwa wa kuchangia chakula mashuleni ili kuwapatia wanafunzi lishe bora wanapokuwa shuleni.
Taarifa zinaonesha kuwa katika robo iliyopita ya Oktoba hadi Desemba 2025, Wilaya ya Kishapu ilikuwa imefikia asilimia 79 ya maadhimisho ya SIku ya Afya na lishe ya kijiji . Hata hivyo, katika robo ya Januari hadi Machi 2026, wilaya hiyo imefanikiwa kufikia asilimia 100.
Maadhimisho ya siku ya afya na lishe ya kijiji yametajwa kuwa miongoni mwa sababu zilizochangia mafanikio hayo, kutokana na elimu iliyotolewa kwa wazazi, walezi na wanafunzi kuhusu umuhimu wa lishe bora mashuleni.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson akizungumza kwenye kikao cha kujadili taarifa za utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya Wilaya, Kata na Vijiji kwa kipindi hicho kikao kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri hiyo Juni 11, 2026
Afisa lishe Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Furaha Kabunwa
Social Plugin