
Na Bora Mustafa, Arusha .
Wananchi wa Mkoa wa Arusha wamehimizwa kujitokeza kwa wingi katika mikutano ya hadhara itakayofanyika wakati wa ziara ya Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, ili kupata fursa ya kuwasilisha kero, maoni pamoja na mapendekezo yao kwa viongozi wa chama na Serikali.
Akizungumza leo 01,June,2026 na waandishi wa habari katika Ofisi za CCM Mkoa wa Arusha, Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa CCM Mkoa wa Arusha, Saipulani Ramsey, amesema maandalizi ya ziara hiyo yamekamilika na wananchi wanapaswa kutumia nafasi hiyo kueleza changamoto zinazowakabili katika maeneo yao.
Amesema ziara hiyo ya siku tatu itaanza Juni 4 hadi Juni 6 mwaka huu, ikiwa na lengo la kusikiliza wananchi, kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kuimarisha uhai wa chama katika ngazi mbalimbali za uongozi.
Kwa upande wake, Ramsey amesema ujio wa Kihongosi ni sehemu ya juhudi za chama za kuhakikisha wananchi wanapata nafasi ya kusikilizwa na kushirikishwa katika masuala ya maendeleo yanayotekelezwa na Serikali chini ya uongozi wa CCM.
Hata hivyo, amesisitiza kuwa mafanikio ya ziara hiyo yatategemea ushiriki wa wananchi wenyewe, akiwataka kujitokeza kwa wingi katika mikutano yote iliyopangwa ili kutoa maoni yao kwa uwazi na kupata majibu ya changamoto zinazowakabili.
Aidha, amesema katika kipindi cha ziara hiyo, Katibu huyo wa NEC atapata nafasi ya kutembelea maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kujionea utekelezaji wa shughuli za maendeleo pamoja na kusikiliza maoni ya wananchi kuhusu huduma zinazotolewa.
Pamoja na hayo, viongozi wa chama na Serikali katika ngazi mbalimbali wanatarajiwa kushiriki katika mikutano hiyo ili kupokea na kufanyia kazi hoja zitakazowasilishwa na wananchi.
Ramsey ametoa wito kwa wakazi wa Arusha kutumia vyema fursa hiyo ya kipekee kwa kufika mapema katika maeneo ya mikutano na kushiriki kikamilifu katika mijadala itakayofanyika wakati wa ziara ya Kihongosi.


Social Plugin