
Baadhi ya wajumbe walioshiriki kwenye uzinduzi wa mradi wa malezi na makuzi ya mtoto unaotekelezwa na Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Shinyanga.
Hatua mpya ya kuimarisha malezi na makuzi ya watoto wenye umri wa kuanzia miaka 0 hadi 3 imeanza mkoani Shinyanga baada ya Katibu Tawala wa Mkoa huo, CP Salum Hamduni, kuzindua rasmi mradi wa malezi na makuzi ya mtoto unaotekelezwa na Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Shinyanga.
Mradi huo unalenga kuboresha maendeleo ya awali ya mtoto kupitia malezi bora, ushiriki wa jamii pamoja na kuimarisha ustawi wa uchumi wa kaya ili watoto waweze kukua katika mazingira salama na yenye fursa za kujifunza.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, CP Hamduni amesema ustawi wa mtoto katika hatua za mwanzo za maisha yake ni msingi muhimu wa kujenga taifa lenye rasilimali watu bora na wenye uwezo wa kuchangia maendeleo ya nchi.
Amesema wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira bora, salama na yanayowezesha ukuaji wa afya ya mwili na akili.
"Kupitia mradi huu tunatarajia kuona ongezeko la uelewa wa wazazi na walezi kuhusu malezi bora ya watoto, pamoja na kuboreshwa kwa afya na lishe ya watoto katika Mkoa wa Shinyanga," amesema CP Hamduni
Ameongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendana na juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita za kuboresha huduma za maendeleo ya awali ya mtoto kwa kuhakikisha watoto wanapata huduma bora za afya na lishe zinazochochea ustawi wao kwa ujumla.
Kwa upande wake, Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Dayosisi ya Shinyanga, Johnson Chinyong’ole, amesema mradi huo utatekelezwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, ukihusisha vijiji vya Mayanji, Bulimba, Mwaweja na Negezi.
Askofu Chinyong’ole amesema utekelezaji wa mradi huo ni sehemu ya kutekeleza wito wa kiimani wa kuhakikisha jamii inakuwa na maisha bora, akisisitiza kuwa afya na ustawi wa mtoto ni msingi wa maendeleo ya jamii.
Ameeleza kuwa mradi huo utatekelezwa kwa ushirikiano wa karibu na jamii pamoja na wadau mbalimbali wa afya ili kuongeza uelewa kuhusu malezi bora, haki za mtoto na umuhimu wa kuandaa mazingira mazuri ya ukuaji wa watoto.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dkt. Honaratha Rutatinisibwa, amesema mradi huo utaisaidia jamii kupata elimu zaidi kuhusu malezi ya mtoto na kuchangia kupunguza tatizo la udumavu pamoja na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto.
Uzinduzi wa mradi huo umehudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo, afya na makuzi ya mtoto, huku ukitajwa kuwa hatua muhimu ya kuongeza uelewa wa malezi bora na kuimarisha ustawi wa watoto katika jamii za Mkoa wa Shinyanga.




Social Plugin