Mamia ya wananchi wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga wamejitokeza kupata huduma za matibabu ya kibingwa bure katika Hospitali ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kupitia kambi maalumu ya afya iliyoratibiwa na Taasisi ya Mo Dewji Foundation.
Baadhi ya Wananchi waliopata na wanaotarajia kupata huduma hizo wameipongeza Serikali pamoja na Mo Dewji Foundation kwa kuwasogezea huduma za kibingwa karibu na makazi yao bila gharama. Wakizungumza wakati wa zoezi hilo Juni 12, 2026, wamesema huduma hizo zimewasaidia kupata uchunguzi, ushauri wa kitaalamu na matibabu ambayo yangehitaji gharama kubwa kuyafuata katika hospitali za rufaa.
Miongoni mwa wanufaika hao, Mrundi Jacobo aliyefika kupata huduma za macho amesema huduma ni nzuri na zimewafikia wananchi wengi, ingawa aliiomba taasisi hiyo kuongeza muda wa utoaji wa huduma kutokana na mwitikio mkubwa wa wananchi. Naye Alex Mushishi alisema ameridhishwa na huduma alizopata ikiwemo kupatiwa miwani na ushauri wa kitaalamu kuhusu changamoto yake ya macho.
Kwa upande wake, mkazi wa Kishapu Sayi Kiyanada ameipongeza Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuwafikishia wananchi wasiojiweza huduma za matibabu bure, huku Maria Charles aliyefika kupata huduma za uzazi akieleza matumaini yake ya kupata suluhisho la changamoto za kiafya zinazomsumbua kwa muda mrefu.
Akizungumza katika zoezi hilo, Afisa Afya wa Mo Dewji Foundation, Joseph Robert, amesema huduma hiyo jumuishi imelenga kupunguza athari za magonjwa mbalimbali ya kibingwa ambayo yamekuwa yakichangia ongezeko la ulemavu, umasikini na vifo katika jamii.
Amesema taasisi hiyo imeamua kutoa huduma za kibingwa bure kutokana na kuongezeka kwa wagonjwa wa magonjwa ya macho, saratani ya shingo ya kizazi na matiti kwa wanawake pamoja na changamoto za kichwa kikubwa na mgongo wazi kwa watoto, hali inayochangia kudorora kwa ustawi wa jamii na uchumi wa mtu mmoja mmoja.
Joseph pia ametoa pongezi kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, Mkuu wa Wilaya hiyo pamoja na wananchi kwa mapokezi mazuri na mwitikio mkubwa walioonesha katika zoezi hilo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Emmanuel Johnson, amesema ujio wa madaktari bingwa umepunguza changamoto ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa, jambo ambalo huongeza gharama na usumbufu kwa wagonjwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga Emmanuel Johnson akizungumzia ujuo wa madatari bingwa zaidi ya 40 wilayani humo kwa ajili ya huduma jumuishi ya matibabu ya kibingwa bure katika Hospitali ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kupitia kambi maalumu ya afya iliyoratibiwa na Taasisi ya Mo Dewji Foundation yaliyoanza juni 12 hadi juni 15, 2026 wilayani humo
Mkurugenzi Johnson Ameongeza kuwa huduma hizo zitasaidia wananchi kupata uchunguzi na matibabu stahiki huku pia zikitoa fursa kwa watumishi wa afya wa Halmashauri kujifunza na kubadilishana uzoefu na wataalamu hao ili kuboresha utoaji wa huduma za afya.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu amesema zaidi ya madaktari bingwa 40 wamefika wilayani humo kutoa huduma hizo, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kunufaika na fursa hiyo. Amesema juhudi hizo zinaendana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo.
Afisa Afya taasisi ya mo Dewji Foundation Joseph Robert Mashafi akizungumza namna taasisi ya Mo Dewji Foundation imedhamiria kutoa huduma jumuishi za kibingwa bure nchini Tanzania alipokuwa kwenye kambi ya Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga hospitali ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete iliyoanza Juni 12 hadi 15, 2026
Sayi Kiyanda mkazi wa Kishapu mkoani Shinyanga
Mahewa Buchulu kutokea Kijiji cha Magalata Kata ya Mwamalasa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Maria Charles mkazi wa Kishapu mkoani Shinyanga
Alex Mushishi mkazi wa Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Mrundi Jacobo Juma mkazi wa Kata ya Kishapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Mdeshi Sungwa Mkilya babu kilemba kutokea Kijiji cha Ikonda wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Lubuga Maige Mashala kutokea Kijiji cha Ikonda wilayani Kishapu mkoani Shinyanga
Kashinje Suluba Mkazi wa Isoso Kata ya kihsapu wilayani Kishapu mkoani Shinyanga

Social Plugin