
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Wizara ya Madini, Dkt. Anold Gesase, amewataka wadau wa sekta ya madini kuingia makubaliano yanayozingatia sheria na kuyasajili katika Tume ya Madini ili yawe na nguvu ya kisheria.
Dkt. Gesase ametoa wito huo wilayani Bukombe, mkoani Geita, alipokuwa akizungumza na washiriki wa mafunzo ya haki za madini na haki za ardhi yaliyowakutanisha wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo, wamiliki wa mashamba, wamiliki wa maduara na wadau wengine wa madini kutoka Mkoa wa Kimadini Mbogwe.
“Usifanye kazi yako kwa maelewano ya mdomo pekee, utakosa ulinzi wa kisheria,” amesisitiza Dkt. Gesase.
Awali, akifungua mafunzo hayo, Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Mbogwe, Mhandisi Jeremiah Hango, aliwakumbusha washiriki kuzingatia haki na wajibu wa kila mmoja katika utekelezaji wa shughuli zao za kila siku.
Mhandisi Hango amesema mafunzo hayo yamelenga kuwaelimisha wamiliki wa leseni za uchimbaji mdogo na wamiliki wa mashamba kuhusu haki na wajibu wao ili kupunguza migogoro inayojitokeza katika sekta hiyo.
“Unakuta mtu ana leseni lakini haendelezi shughuli za uchimbaji, halipii ada ya mwaka (annual rent), na baada ya miaka saba kuisha haji kuhuisha leseni. Leseni inapofutwa kwa mujibu wa sheria, ndipo migogoro huanza,” amesema.
Mafunzo hayo yanalenga kumaliza migogoro ya aina hiyo ili wadau watumie muda mwingi katika uzalishaji badala ya kushughulikia migogoro.







Social Plugin