
“Wananchi Lazima Wapate Haki Yao,” Dk Mwinyi Azindua Awamu ya Pili ya Kampeni ya Mama Samia
“Kipaumbele tulichokiweka tangu kuanzishwa kwa taifa letu ni kuhakikisha wananchi wanapata haki.
Kwa sasa tunaendelea kuweka mifumo bora ya kisheria itakayorahisisha upatikanaji wa huduma hizo,” alisema Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo ilitolewa wakati wa uzinduzi wa Awamu ya Pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia uliofanyika katika Viwanja vya Dole vilivyopo Mkoa wa Mjini Magharibi kule Unguja.
Dk Mwinyi alieleza kuwa serikali imedhamiria kwa dhati kuendelea kuondoa vikwazo vyote vinavyowakwamisha wananchi kupata haki zao za msingi kwa kuimarisha mifumo, miongozo na kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria nchini ili kukuza utawala bora na kulinda haki za binadamu.
Dk Mwinyi alibainisha kuwa tangu kuanzishwa kwa kampeni hiyo ya kipekee mnamo mwaka 2023, imekuwa chachu kubwa ya kuwafikishia wananchi huduma za kisheria na kuwapatia ufumbuzi wa changamoto mbalimbali ambapo katika kipindi cha miaka mitatu hadi kufikia sasa mwaka 2026, zaidi ya wananchi milioni nne wamefaidika nchi nzima.
Mafanikio hayo yamegusa halmashauri 195, vijiji 4,287, kata 229, shehia 388 na mitaa 1,645 ambapo wananchi wamepata huduma mbalimbali zikiwemo utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala, ushauri kutoka kwa mawakili wa kujitegemea na uandaaji wa nyaraka za kisheria.
Kiongozi huyo aliongeza kuwa suala la haki limepewa kipaumbele cha juu kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Ilani ya CCM ya mwaka 2025-2030, na hivyo akasihi wananchi, hasa wa maeneo ya pembezoni, kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo iliyoboreshwa.
Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Juma Homera alifafanua kuwa katika awamu hii ya pili, huduma hizo zitasogezwa karibu zaidi na wananchi wa vijijini pamoja na makundi maalumu wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu. Alisisitiza kuwa watendaji kutoka wizarani na taasisi mbalimbali wapo tayari uwanjani kusikiliza na kutatua kero za kisheria ili kuimarisha uwajibikaji.
Hatua hiyo iliungwa mkono na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Huduma za Kisheria (LSF), Lulu Ng’wanakilala aliyebainisha kuwa taasisi yake imekuwa mstari wa mbele tangu siku ya kwanza kuunga mkono kampeni hiyo kwa lengo la kuhakikisha huduma hizo zinawafikia wananchi wote bila kuacha mtu yeyote nyuma.
Social Plugin