
Na; Mwandishi wetu – Chato
Mkuu wa Wilaya ya Chato Mhe. Louis Peter Bura Amepongeza Programu ya kuendeeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) inayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu kwa Uratibu wa Kituo cha kuendeleza ukuzaji Viumbemaji Rubambagwe Kilichopo wilayani Chato Mkoani Geita kinachosimamiwa na Wizara ya Mifugo na Uvuvi.
Ametoa Pongezi hizo Tarehe 10 Juni 2026 Wilayani Chato alipofanya ziara maalum ya kutembelea kituo hicho akiwa pamoja na timu ya wataalam waliokutana katika Wilaya hiyo wakiwa katika kazi maalum ya kufanya mapitio ya mpangokazi wa Program hiyo.

Mkuu wa Wilaya Bura, alisema kuwa Wilaya yake inawajibu wa kutoa elimu kwa wafugaji kupitia kituo cha Rubambagwe hivyo amewaasa wataalam kutoka katika sekta zinazotekeleza mradi kufanya kazi kwa ushirikianao na Wilaya hiyo, ili kuweza kuleta matokeo chanya katika uchumi wa Wilaya na Taifa kwa Ujumla na Kuongeza mnyororo wa thamani.

“Tutakuwa tunazalisha vifaranga vya samaki pale, haitatosha hiyo pia tutakuwa tunazalisha vyakula vya samaki, na hayo yote yamenipa mimi wakati mzuri na sababu ya kujifunza haya yote, na tunashukuru mradi huu kwenda kwa kasi na ni wakati sasa wa kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja . “Alibanisha
Sambamba na hilo Mkuu huyo wa Wilaya alisisitiza ushirikishwaji mzuri baina ya sekta zinazotekeleza Programu hiyo nchini pamoja na Wilaya husika.’katika dhana nzima ya ushirikishwaji kuna mambo mengi ambayo Wilaya inaweza kuyasimamia na kuyatekeleza kwa ukaribu zaidi, hapa Chato wananchi wanajihusisha Zaidi na uuzaji wa samaki tuna soko kubwa la samaki hapa linaitwa Chato beach, wananchi wanapata chakula na pia wanauza sehemu nyingine nje ya Chato.’ Alifafanua.

Kwa upande wake Mratibu wa Programu Hiyo kutoka Ofisi ya waziri Mkuu Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu, Bw. Salimu Mwinjaka alisema pamoja na mambo Mengine kwa upande wa bahari kuu, Progamu hiyo inakusudia kujenga viwanda vya samaki Tanzania Zanzibar katika eneo la Fungurefu na Wilayani Kilwa Mkoani Lindi na kuweza kukabili hali ya upotevu wa mazao ya samaki baada ya kuvuna kwa kujenga vyumba vya ubaridi vya kuhifadhi mazao ya uvuvi, mitambo wa kuzalisha barafu, vichanja na mahema yakukaushia dagaa au samaki kwa kutumia mionzi ya jua.

Akiongelea kuhusu ufugaji samaki, Bw. Mwinjaka alisema kupitia progamu hiyo kuna vituo vinne ambavyo vipo chini ya Wizara ya Mifugo na Uvuvi ambavyo ni Pamoja na vituo vya kuendeleza ukuzaji viumbemaji cha Rubambagwe kilichopo Wilayani Chato, Mwamapuli Wilayani Igunga, Kingolwira Wilayani Morogoro na kituo cha Ruhila Wilayani Songea.
Akiongea katika ziara hiyo, Afisa Uvuvi Mkuu kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Bi Mkomanile Mahundi alisema kituo cha Kuendeleza Ukuzaji Viumbemaji Rubambagwe kitakuwa na kazi ya kuzalisha na kusambaza vifaranga bora vya samaki aina ya sato na kambale, pamoja na kutoa mafunzo kwa wakuzaji viumbemaji katika maeneo ya mikoa ya Geita, Mwanza, Kagera, Shinyanga, Simiyu na Mara.

Aliongeza kusema pia, baada ya kituo kukamilika kitakuwa na uwezo wa kuchakata chakula cha samaki ambapo itapelekea wigo wa kuongeza ajira kwa wanawake, vijana na watu wenye mahitaji maalum.
“Wizara ya Mifugo na uvuvi kupitia Programu ya Kuendeleza Kilimo na Uvuvi (AFDP) itawezesha uwepo wa dirisha maalum katika taasisi za kifedha kama vile Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) kwa kuwawezesha wakuzaji viumbemaji kupata mkopo yenye riba nafuu ya pembejeo na zana za ukuzaji viumbemaji.” Alisem

Ujenzi wa Kituo hicho cha Rubambagwe umefikia Asilimia 85 mpaka sasa ambapo umehusisha Jengo la utawala, karakana, nyumba za wafanyakazi jengo la kitotoleshi cha samaki, ujenzi wa mabwawa ya kufugia samaki, chanzo cha maji yaani tenki maalum la kutunza maji, kuchuja na kusafirisha maji hayo kwenda kwenye mabwawa ya kufugia samaki, kitotoleshi pamoja na maeneo mengine yanayotumia maji kituoni hapo.
Social Plugin