Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

URUSI KUFUNGUA FURSA ZAIDI ZA UWEKEZAJI TANZANIA, RAIS SAMIA AKUTANA NA PUTIN MOSCOW



Na Beda Msimbe, TBN – Moscow, Urusi

Shirikisho la Urusi limesema litaendelea kufungua fursa mbalimbali za uwekezaji na ushirikiano kwa Tanzania kwa manufaa ya mataifa yote mawili, huku likiahidi kutangaza fursa hizo katika Mkutano wa Kimataifa wa Uchumi unaotarajiwa kufanyika kesho kutwa nchini humo.

Hayo yameelezwa na Rais wa Shirikisho la Urusi, Vladimir Putin, baada ya kufanya mazungumzo rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, jijini Moscow.

Rais Putin amesema Urusi imekuwa ikifuatilia kwa karibu mageuzi ya kiuchumi na kijamii yanayofanyika Tanzania na kuridhishwa na kasi ya maendeleo inayopatikana nchini.

Amesema mazungumzo yake na Rais Samia yamekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili na yamefungua ukurasa mpya wa kuimarisha ushirikiano katika sekta mbalimbali za maendeleo.

Urusi kwa sasa ina miradi takribani 70 nchini Tanzania yenye thamani ya dola za Marekani milioni 434.22, ambayo imechangia kutoa ajira zaidi ya 3,000 kwa Watanzania.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema ziara yake nchini Urusi ni ya kihistoria kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa Tanzania kufanya ziara ya kiserikali nchini humo baada ya kupita zaidi ya nusu karne.

“Ziara yangu ina umuhimu wa pekee wa kihistoria kwangu binafsi na kwa nchi yangu. Imepita zaidi ya nusu karne tangu kufanyika kwa ziara ya mwisho ya kiserikali ya Tanzania nchini Urusi. Hivyo, kwangu hii ni safari ya kihistoria sana kuja Urusi kujadili masuala mbalimbali ya ushirikiano wa pande mbili pamoja na maendeleo endelevu kwa wananchi wetu,” alisema Rais Samia.

Aidha, Rais Samia alimshukuru Rais Putin na Serikali ya Urusi kwa mwaliko huo na ukarimu waliompatia wakati wa ziara yake nchini humo.

Katika mazungumzo hayo, Rais Samia pia alikumbusha mchango mkubwa wa Urusi katika harakati za Tanzania za kupigania uhuru na kumpongeza Rais Putin kwa maadhimisho ya miaka 81 ya Ushindi katika Vita Kuu ya Pili ya Dunia yaliyofanyika Mei 9 mwaka huu.

Rais Samia aliwasili Moscow kwa ziara yake ya kwanza nchini Urusi, ambayo pia ni ziara ya kwanza ya kiongozi wa Tanzania nchini humo katika kipindi cha zaidi ya miaka 50.

Kwa mujibu wa viongozi hao, mazungumzo yao yalijikita katika kuimarisha zaidi uhusiano wa kirafiki na ushirikiano wa muda mrefu kati ya Tanzania na Urusi, pamoja na kubadilishana mawazo kuhusu masuala muhimu ya kikanda na kimataifa yanayoendelea duniani.

Ziara hiyo inatarajiwa kufungua fursa mpya za uwekezaji, biashara, elimu, teknolojia na ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na Shirikisho la Urusi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha na Rais wa Shirikisho la Urusi Mhe. Vladmir Putin katika Ikulu ya Kremlin Jijini Moscow, tarehe 03 Juni, 2026.


Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com